Na. Innocent Kansha- Mahakama
Mkuu
wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania na Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Mhe. Dkt. Angelo Rumisha, amesema kwamba Mahakama ya Tanzania imepokea
kwa furaha kuona Mahakama ya Zanzibar imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka
Benki ya Dunia kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mradi wa Maboresho wenye
lengo la kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Akizungumza
na ujumbe wa Maafisa kutoka Zanzibar uliongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu
Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar Mhe.
Ibrahim Mzee Ibrahim, hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mhe. Dkt. Rumisha
alisema kwamba, Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania kipo tayari
kushirikiana na Kitengo cha maboresho ya Mahakama ya Zanzibar katika
kuhakikisha kinatekeleza majukumu yake.
“Tuwahakikishie
kuendelea kutoa ushirikiano mara zote wa kubadilishana taarifa zote muhimu kwa
kubadilishana uzoefu, kutatua changamoto za utekelezaji endapo zitatokea na
kwamba milango ipo wazi muda wote mtakapohitaji msaada wetu,” alisema Mhe. Dkt.
Rumisha.
Mahakama
ya Zanzibar kama ilivyo kwa Mahakama ya Tanzania imepata mkopo wenye masharti
nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maboresho utakaojulikana
kwa jina la Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar ‘Zanzibar Judiciary
Modernisation Project’ (Zi-JUMP) mradi huo umeidhinishwa na Benki ya Dunia mnamo
tarehe 10 Mei, 2024 na unatarijiwa kuanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2024 hadi
tarehe 1 Julai, 2029. Mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miaka 5.
Akizungumza
wakati wa mafunzo mafupi ya kubalishana uzoefu juu ya utekelezaji wa mradi wa
maboresho yalifanyika kwa siku mbili Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ambaye
pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar Mhe. Ibrahim Mzee
Ibrahim alitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Mahakama ya Zanzibar kwa
ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa na Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya
Tanzania kwa kuwapatia uzoefu mkubwa na kuahidi kufanyia kazi uzoefu huo ili
kuhakikisha kwamba wanafikia malengo ya Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya
Zanzibar.
Aidha,
Mhe. Ibrahim alimwomba Mkuu wa kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania
(JDU) kuendelea kuwapa ushirikiano na uzoefu zaidi pale watakapohitaji kwa kuwa
wanatambua kazi kubwa iliyopo mbele yao.
Vilevile,
Maafisa hao wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama kutoka Zanzibar wakiongozwa na
Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama
Zanzibar Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim walipata wasaa wa walitembelea Mahakama ya
Tanzania kwa ajili ya kushiriki katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maboresho
iliyofanywa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Malawi,
Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan Belete aliyoifanya hivi karibuni na kupata fursa
ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa miradi hiyo.
Baada
ya ziara hiyo ujumbe kutoka Zanzibar uliwasili katika Kitengo cha Maboresho ya
Mahakama ya Tanzania (JDU) kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa
namna ya kusimamia Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho ya Mahakama ‘Citizen-
Centric Judicial Modernisation and Justice Sevice Delivery Project’
unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, kwakuwa Kitengo hicho hadi sasa kina uzoefu wa
miaka 8 ya kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho ya
Mahakama.
Aidha,
ujumbe huo pamoja na mambo mengi ulipitisha kwenye mafunzo mbalimbali ikiwemo namna
bora ya kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho.
Maeneo
mengine waliyojifunza ni kuhusu majukumu ya kitengo cha maboresho ya Mahakama
Tanzania (JDU) na majukumu ya watumishi wa Kitengo hicho.
Vilevile,
ujumbe huo ulijifunza kuhusu namna ya kuandaa maandiko dhana ‘concept notes’,
menejimenti ya masuala ya manunuzi, uandaaji mipango kazi, na masuala ya usimamizi
wa fedha za mradi ‘Financial Management’.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akifafanua jambo wakati wa kikao cha kubadilishana uzoefu baina ya Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania na Zanzibar.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kubadilishana uzoefu baina ya Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania na Zanzibar, kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim akimsikiliza kwa makini.
Timu ya Maboresho ya miradi Mahakama ya Zanzibar ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim wa kwanza kulia wakifuatilia mambo mbalimbali ya kubadilishana uzoefu wakati wa kutekeleza miradi hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni