Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Rorya Mara
Mkuu
wa Wilaya ya Rorya Ndg. Juma Chikoka amesema wilaya yake inakusudia kuwaelimisha
wananchi kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama na namna ya
kuwasilisha malalamiko yao kuanzia ngazi ya Tarafa hadi vitongoji ili waweze
kupata haki.
Akizungumza
jana wakati wa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya
wilaya ya Rorya yanayotolewa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama,
Mkuu huyo wa wilaya alisema anaamini kuwa wanachi watakapoelimishwa
watawasilisha malalamiko yao kwa usahihi na kupata haki zao.
“Tutawaandikia
barua Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na mpaka kwenye ngazi ya vijiji na
vitongoji ili watoe elimu kwa wananchi kuhusu uwepo wa kamati hizi na wananchi
walete malalamiko yao yanayohusu maadili ya Mahakimu”, alisema.
Alisema
wananchi wengi wa wilaya ya Rorya hawafahamu uwepo wa Kamati zinazopokea
malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama na kuwa endapo
watazifahamu kamati hizi ni wazi kuwa Kamati yake itapokea malalamiko kutoka
kwa wananchi.
Aidha,
Ndg. Chikoka alisema atahakikisha kuwa vikao vya Kamati za Maadili vinafanyika
kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa licha ya ufinyu wa bajeti za vikao
hivyo uliopo. ‘‘Mtarajie kuona mabadiliko
makubwa katika wilaya hii ya Rorya”, alisisitiza.
Akizungumzia mfumo wa kielekitroniki unaotarajiwa kuanzishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama hivi karibuni, Ndg. Chikoka alisema mfumo huo utarahisisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili na pia utawawezesha Wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa urahisi zaidi. Hivyo ameishauri Tume kuharakisha uanzishwaji wa mfumo huo.
Kuhusu
mafunzo, Mkuu wa wilaya ameipongeza Tume kwa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa
Kamati za Maadili kwa njia ya kuwafuata walipo kwani njia hiyo inawawezesha
wajumbe kupata muda wa kutosha kujifunza na pia kupata uelewa mpana zaidi.
Watumishi
wa Sekratariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na kazi ya utoaji wa
Elimu kwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya katika mikoa
ya Mwanza na Mara pamoja na wilaya zake kwa lengo la kuziimarisha Kamatti hizo.
Tume ya Utumishi wa
Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa
Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia
Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza
jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni