Jumanne, 21 Mei 2024

IJA YATOA MAJAJI WANNE WA MAHAKAMA KUU TANZANIA.

  

Na Magreth Kinabo – Mahakama 

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) - Lushoto, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, amesema chuo hicho kimefanikiwa kutoa jumla ya Majaji wanne wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Hayo yasemwa hivi karibuni na Mkuu huyo wa Chuo wakati akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami aliyefanya ziara katika chuo hicho, kwa lengo la kujitambulisha ndani ya maeneo yote ya Mahakama ya Tanzania na kufahamu mafanikio yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Sita kupitia chuo hicho ili kuuhabarisha Umma wa Watanzania. 

Akielezea sehemu ya mafanikio hayo Jaji Kihwelo alisema, “Moja ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika chuo chetu ni kuwepo kwa Majaji wanne waliosoma katika chuo hiki, ambao wameteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania ndani ya kipindi cha Serikali hii. Kimsingi wahitimu wa chuo hiki ni wazuri, mbali na Majaji kuna Wasajili wa Mahakama pia.’’ 

Jaji Kihwelo aliyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kufanikiwa kufanya marekebisho ya Sheria ya mwaka 1998 yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita 2022/23 ambapo mamlaka ya Waziri kuteua Wajumbe wa Baraza la chuo hicho yamepelekwa kwa Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Tanzania badala ya Waziri na Waziri kuwa na Mamlaka ya Kisera zaidi. 

Pia aliongeza kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia na kupitisha Muundo mpya wa Chuo, ambapo hivi sasa ndio unaanzisha Kurugenzi ya Mafunzo ya Kimahakama ambayo awali haikuwepo. 

“Chuo kimefanikiwa kutoa mafunzo kwa watu 700 ambao ni Watumishi wa Mahakama katika maeneo tofauti na Wadau wengine kwa kila robo mwaka ya utekelezaji na mafunzo haya yana matokeo chanya kwa kuwa yanaleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwenye maeneo yao ya kazi, kwa mfano mafunzo ya wanyamapori yanayoendelea hivi sasa ambayo tumeyaendesha nchi nzima tulianza na Morogoro, Pwani na kila tunapokwenda tunawapeleka na mbuga za wanyama sasa tuko katika mikoa ya mwisho ya kanda ziwa. Na haya tumeyafanya moja ikiwa ni sehemu kuunga mkono juhudi za Mhe.Rais na Sekta ya Utalii nchini katika kutangaza utalii na pili ni kujifunza elimu ya uhifadhi kwa sababu kule wanajifunza namna wanyama wanavyohifadhiwa na kukabiliana na ujangili,” alisisitiza Dkt.Kihwelo. 

Hali kadhalika, Jaji huyo alisema eneo lingine ambalo Serikali imewekeza chuoni hapo ni katika la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo na wao kama chuo hawajabaki nyuma na eneo hilo la teknolojia limewarahishishia sana utendaji kazi kwa kuwa hivi sasa wanafanya kazi kwa kutumia ofisi mtandao hata kwenye kupitisha masuala ya manunuzi na mengineyo wakiwa mahali popote. 

Vilevile, alisema Serikali imefadhili ujenzi wa Bweni la Wanafunzi kwa asilimia 100 kupitia Mahakama ya Tanzania lijulikanalo kwa jina la ‘Benjamin Mkapa’ lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 wanaoishi kwa usalama zaidi tofauti na makazi ya nje ya chuo na ni moja ya chanzo cha mapato yanayosaidia uboreshaji wa miundombinu mingine na ukarabati wa majengo mbalimbali ya chuo. 

Jaji Kihwelo alieleza kuwa kwa upande wa ajira za Watumishi wa chuo wamefanikiwa kupata Watumishi wa ajira mpya 24 na Watumishi waliohamia chuoni hapo ni 22 hali iliyosababisha kujazwa kwa nafasi muhimu zilizokuwa na changamoto hapo awali ikiwemo TEHAMA, Mipango na Uhasibu. 

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kimekua na mafanikio mengi kwa kipindi hicho ambamo ndani yake ni pamoja na kuongeza kwa idadi ya ajira za watumishi wa chuo kutoka 102 hadi 112 mwaka 2024.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) - Lushoto, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kulia) akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami, kuhusu mafanikio ya Serikali katika Kipindi cha Awamu ya Sita kupitia chuo hicho.


Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami (kulia) akizungumza jambo na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) - Lushoto, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.


Mwonekano wa Jengo la Bweni la Wanachuo lijulikanalo kwa jina la ‘Benjamin Mkapa’ lililojengwa kwa ufadhili wa Serikali chuoni hapo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni