Jumamosi, 11 Mei 2024

JAJI MFAWIDHI KANDA YA DAR ES SALAAM AONGOZA KIKAO KAZI CHA MAHAKIMU WAFAWIDHI

· Asisitiza usimamizi katika kusajili mashauri kwenye mfumo Mahakama za Mwanzo

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ameongoza kikao kazi kwa Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya kilichofanyika leo tarehe 11 Mei, 2024 ili kufanya tathmini ya utendaji kazi na kuimarisha ufanisi.

 

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni, Mhe. Maghimbi amesema kuwa ni vema kwa Viongozi hao kutathmini utendaji wa kazi, mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika mwaka mmoja uliopita ili kuhakikisha haki inatolewa kwa umma kwa njia bora zaidi.

 

“Kuna haja ya kila baada ya mwendo fulani kufanya tathimini tuko wapi, kwa nini tupo hapo tulipo na kama tulipo ni sawa na tufanye juhudi gani kutoka pale tulipo ili twende tukafanye vizuri zaidi,” Mhe. Maghimbi amesema. 

 

Kikao hicho kimeweka malengo mapya, ikiwemo kuhakikisha kutokuwepo kwa mashauri ya muda mrefu kufikia tarehe 30 Mai, 2024 kwa Mahakama zote kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama Kuu.

 

Kadhalika, Jaji Mfawidhi aliwahimiza Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya kutekeleza wajibu wao kama mwongozo unavyosema na kusimamia vyema Mahakama za Mwanzo katika kusajili mashauri kwenye mfumo.

 

Mhe. Maghimbi alitumia fursa hiyo kuwashukuru Mahakimu hao Wafawidhi kwa ushirikiano wao toka alipofika kuhudumu katika Kanda ya Dar es Salaam yapata mwaka mmoja na miezi miwili sasa.

 

“Niwashukuru kwa kujitolea kwenu, nimeona umahili na uwajibikaji wenu na haya ndiyo yamekua msingi wa utendaji mzuri kwa Mahakama yetu. Nawashukuru pia kwa kuleta haki kwa uadilifu kwa jamii yetu. Najua mazingira tunayofanyia kazi siyo rafiki kama vile ambavyo tungependa, lakini mbali ya yote hayo tunajitahidi kupambana na hali kama ilivyo,” amesema  

 

Jaji Mfawidhi pia amewapongeza Viongozi hao kwa uadilifu na kujitolea kwao katika utendaji kazi maana wakati anafika katika Kanda ya Dar es Salaam alikuta mashauri ya mlundikano yakiwa 1,522, lakini sasa yamebaki 233.

 

Aidha, Mhe. Maghimbi amewashukuru Mahakimu Wafawidhi wageni kwani wamepokea kijiti vizuri na wamekwenda kwa kasi ile ile na zaidi ya matarajio.

 

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiongoza kikao kazi kwa Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya. Kushotoni Naibu Msajili Mfawidhi, Mhe. Sundi Fimbo na kulia ni Naibu Msajili, Mhe. Livin Lyakinana.




Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akifuatilia michango ya wajumbe wa kikao.  

 

Wajumbe kikao kazi cha Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya (juu na chini) wakiendelea na kikao.



Naibu Msajili Mfawidhi, Mhe. Sundi Fimbo (kulia) na Naibu Msajili, Mhe. Aziza Mbadjo wakipata maelezo kutoka Kwa Afisa Tehama, Bi. Elisia Meena.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 


 


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni