Ijumaa, 10 Mei 2024

KAMATI YA MAADILI YA MAHAKIMU MKOA WA PWANI YAAPISHWA

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Pwani 

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ameitaka kamati ya maadili ya maafisa wa Mahakama Mkoa wa Pwani kushughulikia malalamiko yanayoletwa mbele yake kwa uadilifu.

 

Mhe. Maghimbi ametoa wito huo leo tarehe 10 Mei, 2024 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani baada ya kumwapisha Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wa kamati hiyo.

 

Jaji Mfawidhi amesema kuwa kamati hizo zipo kisheria na zimeundwa kupitia kifungu cha 66 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama ambacho kinaipa Tume ya Utumishi wa Mahakama mamlaka ya kutengeneza kanuni mbalimbali.

 

Ameeleza kuwa kanuni hizo zinasaidia katika utekelezaji na usimamaizi wa shughuli zinazoendeshwa na Mahakama na kuwasimamia Mahakimu katika utekelezaji wa shughuli zao pindi wanapokiuka miiko na maadili ya Mahakama.

 

Mhe Maghimbi amefafanua kuwa kanuni hizo pia zinaonesha sifa na majukumu ya Mwenyekiti, Katibu na majukumu ya wajumbe.

 

Amesema kuwa kanuni ya tisa inazitaka kamati hizo kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake iliyopewa kuhakikisha wajumbe wanakula kiapo na bila kufanya hivyo yote yatakayokuwa yamejadiliwa yatakua batili. 

 

“Kazi hii ni kubwa sana, hivyo inahitaji usiri, kutokuwa na upendeleo, huba wala chuki kwa upande wowote na kusimamia ukweli uliopatika katika uchunguzi,” Jaji Mfawidhi amesema.

 

Viongozi wa kamati hiyo walioapishwa ni Mwenyekiti, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge na Katibu ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Rashid Chapa.

 

Wajumbe walioapishwa ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, Mkuu wa Mashtaka Pwani, Bi. Faraja Kiula Mchungaji ulius Shelukai, Sheikh Hamis Mtupa na Mtolo Katele.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kulia) akiwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Pwani tayari kwa kuwaapisha Viongozi na wajumbe wa kamati ya maadili. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Viongozi wengine.

Mkuu wa Mkoa Pwani, Mhe Abubakar Kunenge akila kiapo.


 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kulia) akimkabidhi cheti Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge baada ya kumwapisha.


Sheikh Hamis Mtupa akila kiapo mbele ya Jaji Mfawidhi.

 

 

Kamati ya maadili kwa maafisa wa Mahakama Mkoa wa Pwani. Katikati waliokaa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi. Wengine ni Mwenyekiti wa kamati ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge (kushoto). Kutoka kulia waliosimama ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Joyce Mkhoi, Sheikh Hamis Mtupa, Mtolo Katele, Mch. Julius Shelukai na Mkuu wa Mshitaka Pwani, Bi. Faraja Kiula.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)



 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni