Na Paul Pascal –Mahakama Moshi.
Wanachi
wa Kata ya Kwakoa Wilaya Mwanga Mkoani Kilimanjaro wamekabidhi eneo lenye ukubwa
wa hekari Nne (4) kwa Uongozi wa Mahakama ya Wilaya Mwanga kwa ajili ya
kuwezesha kujenga Mahakama ya Mwanzo itakayo wahudumia katika Kata hiyo yenye
jumla ya vijiji 12 na idadi ya watu ipatayo 17,016 kwa mujibu wa Sensa ya watu
na makazi ya mwaka 2022.
Akizungumza
wakati wa mabidhiano ya eneo hilo jana tarehe 9 Mei 2024 Diwani wa Kata ya
Kwakoa Bw. Kiende Athuman Mvungi alisema Kata hiyo ni miongoni mwa Kata Tano
zinazounda Tarafa ya Jipendea ila katika Kata zote hakuna Mahakama ya Mwanzo
hali inayopelekea wananchi kusafiri umbali mrefu. Mfano kutoka kata ya Toloha
hadi ilipo Mahakama ya Mwanzo Lembini ni zaidi ya kilometa 50.
“Tumetoa
eneo hili kuonyesha uhitaji na kiu ya kupata huduma hii muhimu ya haki katika
Kata yetu ya Kwakoa kwa kuwa eneo hili lipo katikati ya Tarafa yetu, hivyo
wananchi wa Kata zote watapata huduma kwa urahisi tukiwa na Mahakama yetu ya Mwanzo
hapa. Niwaombe viongozi wa Mahakama kuona utayari na kiu yetu ya kutaka huduma
ya Mahakama,” alisema Diwani huyo
Aidha,
Mhe. Mvungi alisema, wananchi katika Tarafa hiyo wapo tayari kuanza ujenzi wa
Mahakama hiyo kwa kutumia utaratibu wa msaragambo kama ambavyo tunafanya katika
miradi mingime ya maendeleo katika tarafa hii, akawaomba viongozi wa Mahakama
waliofika kupokea eneo hilo kufikisha kilio hichi kwa uongozi wa Kanda na Taifa
ili kuona namna bora ya kushirikiana nao ili ujenzi huu ufanyike mapema.
Naye,
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mwanga Mhe. Mariam Mfanga aliwashukuru
Viongozi wa Kata hiyo kwa utayari wao na jitihada zao za kuonyesha nia ya dhati
ya kutaka kusogezewa huduma za kimahakama karibu na jamii ili kila mwenye haki
apate haki yake kwa wakati.
“Hii
ni ishara njema ya uungwaji mkono wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa
kupitia ya nguzo ya Pili ya Mpango huo ambao ulianza kutekelezwa toka mwaka
2020/21-2024/25. Nawaahidi dhamira hii mliyoionesha hapa haitofifia nitawasilisha
katika mamlaka zetu zote na kushirikiana nanyi tuweze kufanikisha yote
tuliyojadili na kuafikiana,” alisema Mhe. Mfanga
Kwa
upande wake, Afisa Utumishi Mahakama ya Wilaya mwanga Bw. Amedeusi Tarimo ambaye
alimuwakilisha Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Moshi aliwashukuru na kuwapongeza
wananchi hao kwa kuonyesha imani yao kwa Mhimili wa Mahakama.
“Niwashukuru
viongozi na wananchi wote wa Kata hii hakika mmetutia moyo katika kazi yetu ya
kuhakikisha tunawahudumia watanzania wote kupata haki zao kwa wakati eneo hili
mlilolitoa tumelipokea na niwahakikishie kwa kasi tuliyonayo Mahakama ya
Tanzania italiendeleza kwa wakati na kwa shughuli mlizokusudia,” alisema Bw.
Tarimo.
Shughuli
hiyo ya mabidhiano iliudhuriwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya Mwanga, Afisa
Utumishi Mahkama ya Wilaya ya Mwanga, Mhe. Diwani Kata ya Kwakoa, Mwenyekiti wa
Kijiji cha Kwakoa, Mtendaji Kata ya Kwakoa, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwakoa,
pamoja na wananchi wa Kata hiyo kwa pamoja walisaini Muhtasari na barua za makabidhiano
ya eneo hilo ikiwa ni ishara ya kuimilikisha Mahakama ya Wilaya ya Mwanga kwa
ajili ya ujenzi wa Mahakama na nyumba za watumishi watakaohudumu katika Mahakama
hiyo itakapokamilika.
Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Mwanga Bw.
Amedeus Tarimo akizungumza na wananchi wa Kata ya Kwakoa baada ya makabidhiano
ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kwakoa.
Diwani
wa Kata ya Kwakoa Mhe. Kiende Athumani
akizungumza wakati wa mkutano wa makabidhiano ya eneo kwa ajili ya kuomba
upatikanaji huduma ya Mahakama ya Mwanzo Kwakoa
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga
Mhe. Mariam Mfanga (wa pili kutoka kulia) akisikiliza mazungumzo ya washiriki wa mkutano katika zoezi
la makabidhiano ya eneo kwa ajili ya kuleta huduma za Mahakama ya Mwanzo Kwakoa
Viongozi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga pamoja na Viongozi wa Vijiji na Vitongoji vya Kata ya Kwakoa wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano huo.
Viongozi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga pamoja na Viongozi wa Vijiji na Vitongoji vya Kata ya Kwakoa wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano huo.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni