Ijumaa, 10 Mei 2024

MAJAJI WA RUFANI WAVUTIWA NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA YA MAHAKAMA KIGOMA

 Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

Majaji wa Mahakama ya  Rufani waliopo mkoani Kigoma kwa ajili ya kikao cha kusikiliza mashauri ya Rufani wamewapongeza Viongozi na watumishi wa  Mahakama ya Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma kwa kutunza vema mazingira  ya Mahakama. 

Pongezi hizo zilitolewa jana tarehe 09 Mei, 2024 walipotembelea jengo la Mahakama Kuu Kigoma baada ya kuhitimisha kikao cha kusikiliza jumla ya mashauri 26 yaliyopangwa katika Kituo hicho. 

Aidha, Jaji wa Rufani, Mhe. Zephania Galeba, alisema “hakika kampeni ya upandaji miti na kutunza mazingira Mahakama Kigoma wameiishi vema maana mazingira haya ni kielelezo kuwa viongozi wa Mahakama Kigoma ni wabunifu katika kutekeleza wito wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, ambaye aliutoa kwa kila Mahakama kuweka kipaumbele cha kutunza mazingira na kupanda miti rafiki kwa mazingira.”

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.Dkt. Benhaji Masoud alisema kuwa, Kigoma ni moja ya Mikoa ambayo imependelewa jengo zuri ambalo sio tu kwa shughuli za Mahakama lakini ni kivutio kwa wakazi na wageni na kukiri pia hata wao Majaji walipofika katika Mahakama wamefurahia jengo kubwa ambalo lina mvuto wa aina yake.

 Kadhalika, Mhe Dkt. Masoud amewapongeza Viongozi Wakuu wa Mahakama ya Tanzania kwa uamuzi wao wa kujenga jengo hilo mkoani Kigoma. 

Zoezi ya kuwatembeza Majaji hao katika jengo hilo liliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, ambapo walijionea mandhari nzuri na mifumo mbalimbali iliyopo katika Jengo hilo. 

Aidha, Mhe. Rwizile aliwaeleza Majaji hao kuwa, utunzaji wa Jengo hilo pamoja na miundombinu yake ni kipaumbele cha Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ikiwa ni mkakati wa kuweka mazingira bora, rafiki na wezeshi ya kufanyia kazi kwa watumishi na wadau wanaotumia jengo hilo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (wa kwanza kulia) akiwaongoza sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutembelea jengo la Mahakama hiyo, wa pili kulia ni Jaji wa Rufani, Mhe. Dkt. Benhaji Masoud, wa pili kushoto ni  Jaji wa Rufani,  Mhe. Zefania Galeba na wa kwanza kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Kigoma,  Bw. Festo Sanga.

Picha ya muonekano wa Jengo na mazingira ya Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ambalo limetembelewa na Majaji wa Mahakama ya Rufani waliokuwa katika kikao cha kusikiliza mashauri ya Rufani mkoani humo.

Muonekano wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma  na mazingira yake kwa upande wa nyuma wa jengo.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani waliotembelea jengo la Mahakama Kuu Kigoma. Kushoto ni Mhe. Dkt. Benhaji Masoud na kulia ni  Mhe. Zephania Galeba.

Picha ya pamoja ya Wasaidizi wa Sheria wa Majaji wa Rufani. Katikati ni Mhe. Khalfan Khalfan na wenzake.

Majaji wa Rufani wakipokea maelezo mafupi kutoka kwa Msaidizi wa kumbukumbu, Bi. Neema Ismail (kulia) mara baada ya Majaji hao kutembela Ofisi ya Kumbukumbu na Nyaraka katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni