Ijumaa, 10 Mei 2024

MAAFISA TAWALA, UTUMISHI ARUSHA WANOLEWA JUU YA MFUMO WA 'PSSSF MEMBER PORTAL'

Na Seth Kazimoto -Mahakama Kuu Kanda ya Arusha

Maafisa Tawala na Utumishi wa Mahakama ya Tanzania mkoani Arusha wamepatiwa mafunzo ya Mfumo wa Kusajili na Kuwasilisha Madai ya Mafao kwa njia ya mtandao ili kuwajengea uwezo Maafisa hao waweze kuwafundisha watumishi walio chini yao kutumia Mfumo huo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF).

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo jana tarehe 09 Mei, 2024 yaliyofanyika katika ukumbi wa Kituo hicho, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya alisema mafunzo hayo pia yamelenga kuwawezesha watumishi kuutumia Mfumo huo wa kielektroniki wa kusajili na kuwasilisha madai na mafao mbalimbali ikiwemo fao la uzazi na la kustaafu.

“Ni matarajio yangu kuwa, mafunzo haya yataleta matokeo chanya kwa Mahakama kwani watumishi wataweza kutumia Mfumo husika bila vikwazo na hata likitokea hilo watapata usaidizi wa karibu kwa hawa Maafisa wao wanaowasimamia,” alisema Bw. Chonya.

Mafunzo hayo yametolewa na Maafisa wataalam kutoka Mfuko wa PSSSF Kitengo cha Utekelezaji Arusha ambao ni Kaimu Meneja wa PSSSF Kanda ya Kaskazini, Bw. Venance Mwaijibe na Afisa Utekelezaji wa PSSSF, Bw. Noel Ngayo.

Akitoa elimu kwa Washiriki wa Mafunzo hayo, Bw. Mwaibije alisema kwamba, Mfumo huo unamuwezesha mstaafu kujihakiki akiwa nyumbani kwake, safarini au mahali popote.

Mbali na kutoa elimu juu ya namna ya kusajili na kuwasilisha maombi ya mafao, Bw. Mwaijibe ameeleza kuwa, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) umeanzisha Mfumo wa PSSSF Kiganjani unaomuwezesha mwanachama kupata taarifa za michango yake mahali popote alipo bila kufika katika Ofisi za PSSSF. 

Mafunzo hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa Watendaji wa Mahakama nchini kote kuhakikisha watumishi wote wanajisajili katika mfumo wa PSSSF wa kusajili na kuwasilisha madai ya mafao kwa njia ya mtandao. 

Maafisa walioshiriki katika mafunzo hayo ni Maafisa Tawala na Utumishi kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Arusha, Afisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Maafisa Tawala na Utumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.  

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya akifungua mafunzo ya 'PSSSF Member Portal' kwa Maafisa Tawala na Utumishi wa Kanda hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho jana tarehe 09 Mei, 2024.

Kaimu Meneja wa PSSSF mkoa wa Arusha, Bw. Venance Mwaijibe akitoa mada ya PSSSF MEMBER PORTAL kwa Maafisa Tawala na Utumishi wa Mahakama mkoa wa Arusha tarehe 9 Mei, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Kaimu Meneja wa PSSSF mkoa wa Arusha, Bw. Venance Mwaijibe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Tawala na Utumishi wa Mahakama mkoa wa Arusha wakati wa mafunzo ya 'PSSF Member Portal' jana tarehe 09 Mei, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho. Upande wa kulia walioketi ni Afisa Utekelezaji wa 'PSSSF' Arusha, Bw. Noel Ngayo na kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Arusha, Bi. Grace Kapama.

 
Maafisa Tawala na Utumishi wa Mahakama Mkoa wa Arusha wakipatiwa mafunzo ya  'PSSSF Member Portal' jana tarehe 09 Mei, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni