Alhamisi, 9 Mei 2024

MKANDARASI WA UJENZI WA JENGO LA ‘IJC’ SINGIDA AKABIDHIWA ENEO LA MRADI

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Makabidhiano ya eneo kwa ajili ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Singida yamefanyika leo tarehe 09 Mei, 2024 huku yakishuhudiwa na wawakilishi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mhakiki Mali wa Mkoa huo pamoja na Viongozi wa Mahakama katika Mkoa huo. 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kikao cha makabidhiano, Mhandisi Mshauri (Consultant) Arch. Rose Nestory, Mradi huo ni wa miezi tisa (9) pekee na utekelezaji wake unaanza rasmi leo na unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa tarehe 08 Februari, 2025.

Mhandisi Rose amesisitiza mambo mbalimbali kwa Mkandarasi wa Mradi ikiwemo kuzingatia muda kwani Mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Benki ya Dunia. Aidha, amesisitiza kuhusu uzalishaji taka kuzingatia kanuni zake katika kuharibu taka hizo. 

Kadhalika, amemsisitiza Mkandarasi kuzingatia mikataba ya ajira kwa vibarua atakaowatumia, kujisajili Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), kutembelea Ofisi ya Manispaa kuonana na Mhandisi wa Manispaa na kuwaona Idara ya Zimamoto kabla ya kuanza shughuli za ujenzi.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa Singida, Bw. Yusuph Kasuka amesema kuwa, Kituo hicho kinategemewa kujengwa ilipokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida Mtaa wa Bomani ambapo amesema jengo hilo la zamani linatarajiwa kubomolewa hivi karibuni kupisha ujenzi wa jengo jipya la kisasa. 

“Taratibu za kuhamisha huduma za Mahakama zimeshafanyika kwa sasa Mahakama ya Hakimu Mkazi inatoa huduma zake katika jengo la kupanga katika Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Singida ‘Complex’ na Mahakama ya Wilaya inafanya shughuli zake katika Mahakama ya Mwanzo Utemini iliyopo mjini hapa,” amesema Bw. Kasuka.

Ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkandarasi na kuhaidi kumtambulisha kwa Taasisi zinazoizunguka Mahakama ili kufahamu uwepo wake. 

Naye Afisa Mazingira kutoka Makao Makuu ya Mahakama, Bw. Castory Kyula amemsisitiza Mkandarasi juu ya utunzaji wa mazingira katika kipindi chote cha ujenzi na kudhibiti kelele kwani eneo la Mahakama linapakana na Ofisi nyingine za Serikali.

Mradi huo wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida unatekelezwa na Kampuni ya ‘Deep Construction Ltd’- Morogoro.
Mhandisi Mshauri, Arch. Rose Nestory (wa tatu kushoto)  akimkabidhi  cheti cha makabidhiano ya eneo 'site' Mkandarasi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 'IJC' Singida. Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 09 Mei, 2024.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka (wa nne kulia) akipokea nakala ya cheti cha makabidhiano ya Mradi wa Ujenzi kutoka kwa Mhandisi Mshauri, Arch. Rose Nestory.
Mhandisi Mshauri, Arch. Rose Nestory (aliyeinama kushoto) Mkandarasi wa ujenzi, Bw. Rabinder Singh (katikati) na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka wakisaini cheti cha makabidhiano ya Mradi (Certificate of site handover to the Contractor).
Wawakilishi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakishuhudia makabidhiano ya eneo la Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida.
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria makabidhiano ya eneo 'site' ya ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni