Jumapili, 26 Mei 2024

JAJI MKUU WA TANZANIA AFANYA MAZUNGUMZO NA JAJI MKUU WA IRELAND YA KASKAZINI

Na Mwandishi wetu, Belfast-Ireland ya Kaskazini

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma amekutana na kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu wa Ireland ya Kaskazini, Mhe. Dame Siobhan Keegan alipomtembelea ofisini kwake Mjini Belfast, Ireland ya Kaskazini. 

Katika mazungumzo na Jaji Mkuu wa Ireland yaliyofanyika tarehe 24 Mei, 2024 Jaji Mkuu wa Tanzania amemshukuru huyo kwa kumpa mwaliko yeye pamoja na ujumbe wake ili pamoja na mambo mengine waweze kushuhudia utiaji saini wa makubaliano katika ya Bodi ya Mafunzo ya Kimahakama ya Ireland ya Kaskazini (Judicial Studies Board of Northern Ireland) na Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha ‘Queens’ Belfast (School of Law Queen’s University Belfast).

Makubaliano hayo yana lengo la kuanzisha Chuo cha Mahakama nchini Ireland ya Kaskazini kwa ajili ya mafunzo kwa Majaji na Mahakimu lakini pia tafiti. 

Mhe. Prof. Juma alisisitiza kuwa yeye pamoja na ujumbe wake wamejifunza mambo mengi kufuatia ziara ya Ireland ya Kaskazini na ukizingatia kuwa Tanzania na Ireland zote ni wanachama wa Jumuiya ya Madola na wana historia inayofanana kwa vile wote wanatumia Mfumo wa Kiingereza yaani ‘Common Law System’.

“Hata hivyo kuna maeneo mengi ambayo Ireland wako mbali ikiwemo kuachana na Sheria zilizotungwa miaka ya 1950,” alisema Jaji Mkuu wa Tanzania. 

Kwa upande wake, Mhe. Dame Siobhan Keegan alisema kuwa, ziara ya Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na ujumbe wake imekuwa na mafanikio makubwa sio tu kwa ujumbe kutoka Tanzania bali hata wao kwa vile wamejifunza mambo mengi ikiwemo maboresho makubwa yanayoendelea katika Mahakama ya Tanzania yenye lengo la kuboresha utoaji haki. 

“Tanzania na Ireland ya Kaskazini ni Nchi ambazo zina historia inayofanana kwa vile zote zinafuata Mfumo wa Kiingereza yaani ‘Common Law System na hivyo kila upande una kitu cha kujifunza kutoka upande mwingine na hivyo, kufuatia mazungumzo haya Ireland ya Kaskazini imegundua kuwa kuna mengi ya kujifunza,” alieleza Jaji Mkuu wa Ireland ya Kaskazini.

Aliongeza kuwa, miongoni mwa mambo waliyojifunza ni pamoja na kuwepo kwa Chuo cha mafunzo ya Kimahakama kwa muda mrefu tofauti na Ireland ya Kaskazini ambayo ina Bodi ya Mafunzo yenye wajibu wa kumshauri Jaji Mkuu kuhusu mafunzo. Aliongeza kuwa Tanzania na Ireland ya Kaskazini zote zinaamini misingi ya utawala wa sheria pamoja na uhuru wa Mahakama. 

Jaji Mkuu wa Tanzania anafanya ziara Ireland ya Kaskazini pamoja na Jamhuri ya Ireland kwa mwaliko wa Jaji Mkuu wa Ireland ya Kaskazini na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Ireland ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama huru katika Jamhuri ya Ireland. 

Vile vile atapa fursa ya kutoa muhadhara kwenye Taasisi ya Kimataifa na Masuala ya Jumuiya ya Ulaya (Institute of International and European Affairs). 

Safari hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubalino kati ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Taasisi isiyo ya kiserikali ya nchini Ireland, ‘Irish Rule of Law International’, makubalino hayo yana lengo la kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama kutoka Tanzania, Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania. 

 Jaji Mkuu  ameambatana na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dr. Paul Kihwelo pamoja na Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na  Jaji Mkuu wa Ireland Kaskazini, Mhe. Dame Siobhan Keegan baada ya kuitembelea Maktaba ya Mahakama ya Ireland Kaskazini tarehe 24 Mei, 2024. Kushoto ni Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Jaji Mkuu wa Ireland Kaskazini, Mhe. Dame Siobhan Keegan (kulia) akimuelezea jambo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) wakati alipotembelea Maktaba ya Mahakama hiyo tarehe 24 Mei, 2024. Katikati ni Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimsikiliza Katibu wa Bodi  ya Mafunzo ya Kimahakama ya Mahakama ya Ireland Kaskazini, Bw. Terence Dunlop alipokuwa akimuelezea jambo kuhusu Bodi hiyo.

Jaji Mkuu wa Ireland Kaskazini, Mhe. Dame Siobhan Keegan (wa pili kushoto) akimtambulisha kwa Jaji Mkuu wa Tanzania (wa kwanza kulia) Wakili aliyekuwa akitumia Maktaba ya Mahakama hiyo kufanya tafiti kabla ya kuingia mahakamani. Wa pili kulia ni Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Mafunzo ya Kimahakama na pia Jaji wa Rufani wa Mahakama ya Ireland Kaskazini, Mhe. John Bernard McCloskey baada ya kufanya mazungumzo naye katika kikao kifupi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Mahakama hiyo tarehe 24 Mei, 2024.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto) akiwa katika kikao kifupi na  Mwenyekiti wa Bodi ya Mafunzo ya Kimahakama ambaye  pia Jaji wa Rufani wa Mahakama ya Irelan Kaskazini,  Mhe. John Bernard McCloskey (wa pili kushoto). Pamoja naye ni Jaji wa Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (wa pili kulia) na Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa. 

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma) 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni