Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga mewataka Maafisa Mahakama kulinda utu na
haki za mashahidi wa mashauri ya unyanyasaji wa kinjinsia wanaposikiliza
mashauri hayo bila kutonesha majeraha ya unyanyasaji wa kinjinsia.
Akifungua mafunzo ya namna bora ya kuepuka
kutonesha majera ya kisaikolojia kwa waathirika wa ukatili wa kingono na kijinsia
jana tarehe 27 mei, 2024 kwa Mahakimu 14 na Maafisa ustawi wa Jamii, yanayofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza, Mhe.
Dkt. Kilekamajenga aliwasihi Mahakimu hao wakiwa kama Maafisa wa Mahakama wana
jukumu la kuhakikisha kuwa haki inatendeka bila kuathiri watu waliopata madhara
yaliyotokana na unyanyasaji.
“Mnapotoa
haki hakikisheni mnatimiza wajibu wenu, huku mkilinda utu na haki za watu wote
wanaohusika katika mnyororo wa haki. Ni marajio ya Mahakama kwamba mwisho wa mafunzo haya yatawajengea ujuzi na
maarifa mtambuka katika kushughulikia mashauri hayo kwa uangalifu na uwelewa
bila kusababisha mathara ya kisaikolojia kwa
wote ambao wamepatwa na madhara ya unyanyasaji wa kijinsia…
Kwa
kuzingatia itifaki za kisheria pamoja na viwango vya maadili ambavyo ni muhimu
katika fani yetu, mafunzo haya yatutujengea uelewa wa sheria na miongozo ambayo
imeweka kwa ajili ya kumlinda shahidi ambaye ni muathirika kwa ujumla kwenye
mashauri yanayohusu unyanyasaji wa kingono. Kupitia msingi huo tutakuwa
tunaimarisha kanuni ya haki ambayo ndiyo msingi mkuu wa mfumo haya,” alisema
Mhe. Dkt. Kilekamajenga.
Mafunzo
hayo yaliyoratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) pamoja na
Irish Rule of Law International (IRLI) yanafanyika kwa muda wa siku tatu (3) yakiwa
na lengo la kuwajengea Mahakimu uelewa wa kutonesha juu ya majeraha ya
kisaikolojia na kuimarisha umuhimu wa kushughulikia mashauri hayo.
Lengo
lingine la mafunzo hayo ni kuimarisha ujuzi wa kuchukua ushahidi unaokubalika
na kuhakikisha kuwa itifaki za kisheria na viwango vya maadili vinafuatwa ili kulinda
utu na uadilifu wa mashahidi na pia kuchangia kufikia maamuzi ya haki na sawa.
Vilevile kuhakikisha kuwa mtuhumiwa anashughulikiwa kwa kuzingatia misingi ya haki.
Mafunzo
hayo yanaendeshwa na wawezeshaji ambao ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mwanza Mhe. Wilbert Chuma, pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Tabora Mhe. Pamela Mazengo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akifungua mafunzo ya namna bora ya kuepuka kutonesha majera ya kisaikolojia kwa waathirika wa ukatili wa kingono na kijinsia jana tarehe 27 mei, 2024 kwa Mahakimu 14 na Maafisa ustawi wa Jamii, yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Mhe. Wilbert Chuma na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya mwanza Mhe. crecensia kisongo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni