Jumatano, 15 Mei 2024

KAMATI ZA MAADILI NA TUME ZATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO

 Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mwanza

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama na Tume ya Utumishi wa Mahakama kutawezesha  Kamati hizo kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kusimamia Maadili na nidhamu ya Mahakimu.


Katibu wa Tume ameyasema hayo jana tarehe 14 Mei, 2024 jijini Mwanza wakati wa utoaji Elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya wakiwemo Wakuu wa wilaya na Makatibu Tawala wa wilaya wa wilaya za Nyamagana, Sengerema, Ilemela na Misungwi.


Alisema endapo ushirikiano kati ya wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama na Tume ya Utumishi wa Mahakama utaimarishwa zaidi, kazi ya kusimamia haki za Watanzania itasonga mbele na wananchi watapata haki kwa wakati.


“Rais Samia Suluhu amekuwa akisisitiza mara zote kuwa tufanye kila linalowezekana ili mwenye haki apate haki na asiye na haki asipate haki”, alisema Mtendaji Mkuu wa Mahakama ambaye pia ni Katibu wa Tume.


Alisema endapo Wajumbe wa Kamati za Maadili watatekeleza ipasavyo jukumu lao la kusimamia Maadili na nidhamu ya Mahakimu, ni wazi kuwa hata wilaya nazo zitatawalika vizuri kwa kuwa ili wilaya zitawalike vizuri ni lazima mnyororo wa utoaji haki nao ukae vizuri.


Aidha, alitoa rai kwa Wajumbe hao kuwawekea Mahakimu mazingira mazuri wanapotekeleza jukumu lao la msingi la kutoa haki, kuwatia moyo na kuwapongeza pale wanapofanya vizuri na endapo watapotoka hawana budi kuwaelekeze kwa utaratibu mzuri.


Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya amewashauri Viongozi wa Kamati za Maadili kujenga utamaduni wa kukabidhiana vitendea kazi zikiwemo nyaraka muhimu pindi wanapohamishwa vituo vya kazi. Alisema kwa kufanya hivyo, anayekabidhiwa ofisi atafahamu nini cha kufanya na pia mwenzake ameishia wapi katika jukumu hilo la kusimamia Kamati hizo.


Naibu Katibu pia amewakumbusha wajumbe hao kuhahakikisha wanaapishwa na Majaji Wafawidhi kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao ya usimamizi wa Maadili na nidhamu ya Maafisa Mahakama. Aliongeza kuwa endapo Wajumbe hawatakuwa wamekula kiapo, shauri watakalolitolea uamuzi nalo litakuwa ni batili.


Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.


Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia), Mkuu wa wilaya ya Sengerema na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya wilaya hiyo Bi. Senyi Ngaga (katikati) na Naibu Katibu wa Tume (Maadili na Nidhamu) Bi Alesia Mbuya wakifuatila jambo wakati wa utoaji Elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya jana jijini Mwanza. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa Mada wakati wa Utoaji Elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya, jana jijini Mwanza. 

Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya akisisitiza jambo wakati wa utoaji Elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya,  jana jijini Mwanza. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati), Naibu Katibu wa Tume (Maadili) Bi. Alesia Mbuya wakiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya za Misungwi, Sengerema na Nyamagana wakati wa utoaji Elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya, jana jijini Mwanza. Aliyekaa kulia ni Katibu Tawala wilaya ya Misungwi Bw. Abdi Makange. Waliosimama kushoto ni Mariam Msengi (Nyamagana) na kulia ni Bw. Cuthbert Midala (Sengerema). 


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za wilaya za Nyamagana na Ilemela  wakati wa utoaji Elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya, jana jijini Mwanza. Waliokaa kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Misungwi Bw. Abdi Makange. 







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni