Jumatano, 15 Mei 2024

MTENDAJI MKUU ATETA NA VIONGOZI, WAWAKILISHI WA TUGHE

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 15 Mei, 2024 amekutana na Viongozi na Wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE kutoka katika Kanda zote za Mahakama nchini na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick, Mkurugezi Msaidizi Utawala, Bw. Steven Magoha na Viongozi wa Taifa wa TUGHE wa Mahakama, Bi. Alice Haule, ambaye ni Mwenyekiti na Alquine Masubo, ambaye ni Katibu.

Viongozi wa TUGHE wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Sara Rwezaura, ambaye ni Mwenyekiti na Bw. Samwel Nyungwa, ambaye ni Katibu, nao walihudhuria mkutano huo uliofanyika kwenye moja ya kumbi zilizopo katika jengo jipya la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, maarufu Judiciary Square.

Wakati wa mkutano huo, Viongozi na Wawakilishi hao wa TUGHE waliwasilisha hoja mbalimbali ambazo zilijibiwa kwa ufasaha na Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania.

Viongozi na Wawakilishi hao walionekana kuridhishwa na namna hoja zao zilivyojibiwa huku Viongozi wa TUGHE Mkoa wakiupongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa namna unavyoshughulikia na kutatua changamoto kadhaa na maslahi ya watumishi.

Walionesha pia kufurahishwa jinsi Uongozi unavyojali watumishi, hasa wa kada za chini katika kuwaendeleza kielimu ambapo miezi michache iliyopita Mahakama ya Tanzania ilitumia takribani Shilingi za Kitanzania bilioni 2.5.

Mkutano huo umekuja siku moja kabla ya kufanyika kwa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, ambalo huwaleta Viongozi wa Mahakama na Wawakilishi wa Chama cha TUGHE kuzungumza mambo mbalimbali ya kiutumishi na kimahakama. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Viongozi na Wawakilishi wa TUGHE kutoka Kanda mbalimbali za Mahakama ya Tanzania.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akizungumza wakati anajibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Viongozi na Wawakilishi hao wa TUGHE.

Katibu wa TUGHE wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Alquine Masubo akiwasilisha baadhi ya hoja kwenye mkutano huo.


Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) ikichukua hoja mbalimbali za Viongozi na Wawakilishi wa TUGHE. Wengine ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick (kulia) na Mwenyekiti wa Mahakama Taifa,Bi. Alice Haule.



Sehemu ya Viongozi na Wawakilishi wa TUGHE kutoka Kanda mbalimbali za Mahakama ya Tanzania (juu na chini) wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri wakati wa mkutano huo.


Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wawakilishi wa TUGHE (juu na picha mbili chini).





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni