Jumatano, 15 Mei 2024

MGOGORO WA MIPAKA YA ARDHI MAHAKAMA YA MWANZO KISESA WAMALIZIKA

  • §  Mahakama Simiyu yawaachia eneo wananchi walilovamia
  • §  Yaomba asitokee mwingine kuingilia eneo la Mahakama

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita leo tarehe 15 Mei, 2024 amefanya ziara katika Wilaya ya Meatu na kufanikiwa kutatua mgogoro wa mpaka wa ardhi uliokuwepo kwa miaka 13 kati ya Mahakama ya Mwanzo Kisesa na Serikali ya Kijiji cha Kisesa.

Bw. Kanyairita aliambatana na Afisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bi. Naumi Shekilindi na Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Meatu, Bw. John Mandisi katika ziara hiyo. 

Mgogoro huo wa ardhi baina ya pende hizo mbili ulianza toka mwaka 2011 ambapo Serikali ya Kijiji iliuza na kugawa eneo la Mahakama kwa wananchi wa Kijiji hicho lenye ukubwa wa takribani heka moja.

Baada ya Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu kufika katika eneo husika, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kisesa, Mhe. Sperancia Sang’udi alionyesha mipaka ya eneo la Mahakama pamoja na maeneo yaliyovamiwa na wananchi.

Kufuatia hatua hiyo, Bw. Kanyairita pamoja na ujumbe wake waliitisha kikao pamoja na Serikali ya Kijiji ili kutatua mgogoro uliokuwepo.

Baada ya mazungumzo kufanyika katika kuimarisha uhusiano mwema na wadau, maridhiano yalifikiwa ambapo wananchi waliachiwa maeneo waliyokwisha kujenga na Mahakama kubakiwa na eneo lenye ukubwa wa heka moja na robo.

Kitendo hicho cha kizalendo kiliibua shangwe na nderemo ziliwawajaa wananchi pamoja na Viongozi wa Serikali ya Kijiji mara baada ya Mtendaji wa Mahakama kutatua mgogoro huo uliodumu kwa takribani miaka 13.

Serikali ya Kijiji na wananchi walimshukuru Mtendaji wa Mahakama kwa kazi kubwa aliyoifanya. “Hatukutegemea kama mgogoro huu ungeweza kuisha kirahisi hivi..

“…tumekuwa tukivutana kwa muda mrefu bila mafanikio lakini leo tumefika tamati tena kwa amani kabisa, tunakushukuru sana Mtendaji na sisi tunakuahidi kukupa ushirikiano wakati wote hata katika hatua ya ujenzi wa Mahakama hii,” mwananchi mmoja alisikika akisema kwa furaha.

Naye Mtendaji wa Mahakama aliwashukuru wananchi na Serikali ya Kijiji kwa ushirikiano walioutoa kwa kuja kuhudhuria kikao hicho na kutenga mipaka ya eneo hilo kwa ajili ya wananchi na Mahakama. 

Aliwaomba wananchi na Serikali ya Kijiji kulilinda eneo la Mahakama na asitokee mtu yoyote wa kuvamia tena eneo hilo, kwani huduma ya Mahakama inayotolewa ni kwa ajili yao wenyewe.

 





Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita akiongea na wananchi pamoja na Serikali ya Kijiji baada ya maridhiano.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita akiwa tayari kwa kuanza kuchimba mipaka.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita akiongea na Viongozi wa Serikali ya Kijiji.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni