Alhamisi, 16 Mei 2024

MASHAURI 24 YA MAUAJI KUSIKILIZWA NA KUAMRIWA MBEYA

Na Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya

Jumla ya mashauri 24 ya mauaji yanatarajiwa kusikilizwa mfululizo na kuyatolewa uamuzi katika kipindi cha mwezi mmoja cha kusikiliza mashauri hayo yatakayoendeshwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya na kufanya jumla ya vikao hiyo kufikia 5 kwa mwaka 2024.


Akitoa taarifa ya ufunguzi wa vikao hivyo hivi karibuni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, alisema kuwa, vikao viwili vitafanyika ndani ya Wilaya ya Mbeya na kikao kimoja kitafanyikia wilayani Rungwe ambapo jumla ya mashauri 24 ya mauaji yanatarajiwa kushughulikiwa katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe 20 Mei, 2024.


Mhe. Temu ameongeza kuwa, mashauri 10 yanatoka Mkoa wa Songwe, mashauri 14 yanatoka Mkoa wa Mbeya. Aidha amewaambia wadau kwamba matarajio ya Mahakama ni kuhakikisha mashauri hayo yanakamilika kwa asilimia 100 kama yalivyopangwa.


“Mashauri yote yamepangwa kwa kuzingatia umri wake toka kusajiliwa mahakamani kwa kitaalamu tumetumia mfumo wa ‘FIFO’ na kesi hizo zinatoka katika Mikoa ya Songwe na Mbeya kwa kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya inaundwa na Mikoa ya Mbeya na Songwe. Hivyo katika mashauri yaliyopangwa kusikilizwa, mashauri 10 yanatoka Mkoa wa Songwe na mashauri 14 yanatoka mkoa wa Mbeya,” alisisitiza Mhe. Temu.


Mhe. Temu amebainisha kuwa mashauri tajwa hayahusishi mashauri yanayosubiri washtakiwa kusomewa kwa mara ya kwanza (plea taking). 

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Dunstan Ndunguru amewashukuru wadau kwa ushirikiano waliouonesha na kuomba kuendeleza ushirikiano huo hasa katika ushiriki wa vikao kama hivyo.


“Vikao kama hivi vimekuwa vikifanikiwa kwa kiasi kikubwa na hutumika katika kujenga ushirikiano mzuri na utatuzi wa mashauri ya mlundikano na yale yenye viashiria vya kuwa mlundikano. Ndiyo vikao pekee ambavyo vinaleta ufanisi mkubwa katika umalizaji wa mashauri yanayokua yamepangwa kusikilizwa kwa mfululizo (sessions),” alisema Jaji Mfawidhi


Aidha, Mhe. Ndunguru amewapongeza wadau kwa ushirikiano ambayo wamekuwa wakiuonesha katika kufanikisha usikilizwaji wa mashauri na kuendelea kuwasisitiza Mawakili na Wadau kutumia utaalamu wao kwa kusoma majalada vizuri na kuongea na wateja wao mapema angalau wiki moja kabla ya kuanza kusikilizwa kwa mashauri yao. Vilevile amewasisitiza Magereza kuhakikisha Mahabusu ambao wako mbali kuwa wanafikishwa mapema angalau wiki moja kabla ya kikao kuanza ili waweze kupata muda wa kutosha kuzungumza na Mawakili wao.


Sambamba na hayo, Wadau kwa pamoja wamehaidi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa na kusema kwamba wao wamejipanga vizuri hasa Ofisi ya Mashtaka katika kuhakikisha mashahidi wao wanapatikana kwa wakati wanaokua wameitwa mahakamani. Wameipongeza Mahakama kwa kuandaa vikao kama hivyo vyenye kuleta tija katika dhana nzima ya utoaji haki kwa wakati.

                                                         

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) akieleza jambo wakati wa kikao kazi na wadau cha maandalizi ya kusikiliza mashauri ya mauaji. Wengine ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu (kulia) na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu akitoa maelezo ya jumla ya utaratibu wa kuendesha vikao vya mashauri ya mauaji katika kanda hiyo.

 Sehemu ya Wajumbe wa kikao hicho ambao ni wadau mbalimbali wa Mahakama wakifuatilia kwa umakini hoja za kikao hicho

 Sehemu ya Wajumbe wa kikao hicho ambao ni wadau mbalimbali wa Mahakama wakifuatilia kwa umakini hoja za kikao hicho

Sehemu ya Wajumbe wa kikao hicho ambao ni wadau mbalimbali wa Mahakama wakifuatilia kwa umakini hoja za kikao hicho


 Sehemu ya Wajumbe wa kikao hicho ambao ni wadau mbalimbali wa Mahakama wakifuatilia kwa umakini hoja za kikao hicho

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni