Ijumaa, 17 Mei 2024

MAHAKAMA YA TANZANIA HAIKAMATIKI KWENYE MABORESHO KATIKA UTOAJI HAKI

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani, hatua ambayo imesaidia kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na utoaji haki kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha alipokuwa anawasilisha mada leo tarehe 17 Mei, 2024 kwenye Baraza Kuu la Wafanyakazi linalofanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini hapa.

Mada iliyowasilishwa inahusu hali ya utekelezaji wa mifumo ya TEHAMA katika uendeshaji wa Mahakama Mtandao. Mhe. Kamugisha ameeleza kuwa moja ya maeneo ya maboresho ya Mahakama ni kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kupitia matumizi ya TEHAMA.

“Ili kutekeleza hili, Mahakama imejenga mifumo kadhaa ya TEHAMA, ukiwemo Mfumo wa Manejimenti ya Mashauri (CMS) na Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS),” Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri ameliambia Baraza la Wafanyakazi.

Mhe. Kamugisha amebainisha kuwa CMS imejengwa kwa nia ya kurahisha shughuli zote za ufunguaji, usikilizaji, usimamizi na uratibu wa mashauri na kuondokana na matumizi ya karatasi katika shughuli hizo. Mfumo huu ulianza kutumika tarehe 06 Novemba, 2023.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amewaeleza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kuwa mwanzoni mwa matumizi ya Mfumo huo ziliibuka changamoto kadhaa, ikiwemo kuchelewa kwa zoezi la kuifungamanisha na Mfumo wa Kielektoniki wa Malipo Serikalini zaidi ya ilivyotarajiwa.

Changamoto nyingine ni baadhi ya watumiaji kutoupokea na kuukubali mfumo kwa kuwa ulibadilisha mtindo wa kazi ambao ulizoeleka kwa muda mrefuna watumiaji wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha wa mfumo. 

“Asilimia 76.61 ya changamoto zilizopokelewa kutoka kwa watumiaji zilihusiana na uelewa wa mfumo na asilimia 23.39 ya changamoto zilihusiana na utendaji wa mfumo,” Mhe. Kamugisha amesema. 

Ameeleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa mfumo huo, maboresho kadhaa yamefanyika, ikiwemo kuuwezesha kutoa taarifa za hatua za shauri kwa wateja kwa njia ya ujumbe wa simu.

Mengine ni kuboresha utaratibu wa malipo, kuwezesha uandaaji wa tuzo na amri kupitia mfumo, kutenganisha maamuzi yasiyomaliza shauri na yale yanayo maliza shauri na kuwawezesha Watunza Kumbukumbu Wasaidizi kuona jalada la kieletroniki ili kurahisisha uandaaji wa wito (summons) na huduma kwa wateja.

“(Mfumo pia) umewezesha utaratibu wa mashauri ya mwenendo wa ukabidhi, umewezesha ufunguaji wa mashauri ya zamani ambayo hayapo kwenye mfumo (na) kuwezesha uingizaji wa mwenendo na hukumu za mashauri ya zamani,” Mhe. Kamugisha amesema.

Kadhalika, kumekuwepo na maboresho ya utaratibu wa mashauri katika mamlaka ya nyongeza, maboresho ya programu-tumizi ya Mahakama za Mwanzo, maboresho ya eneo la coram na mwenendo na ujenzi wa kitu kinachojulikana kama “Judiciary e-service portal.”

Kwa upande wa Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Mfumo huo umewezesha uandishi wa hukumu kwa jopo, umewezesha ubadirishanaji wa rasimu ya hukumu miongoni mwa wanajopo na kuboresha utaratibu wa upangaji mashauri kwa Jaji au Jopo na kwa Naibu Wasajili.

Maboresho mengine ni kuwezesha Jaji wa Mahakama ya Rufani kuandika notisi zake mwenyewe, kuwawezesha Naibu Wasajili kusoma, kutangaza hukumu na kumaliza shauri kwenye mfumo, kuahirisha mashauri bila kuweka tarehe na utoaji wa taarifa kwa Mahakama za chini pale Mahakama ya Rufani inapotoa amri ya shauri kusikilizwa upya.

“Tumefanikiwa pia kuwakutanisha wadau wa mfumo na timu ya ujenzi ili kujadili kwa pamoja changamoto za mfumo,” Mhe. Kamugisha amesema.

Anasisitiza kuwa TTS na CMS ni mifumo muhimu katika kuongeza tija na ufanisi katika usikilizaji wa mashauri na inapunguza muda na gharama za kusikiliza shauri, kuongeza uwajibikaji na uwazi.

Hata hivyo, ili kuwa na matokeo tarajiwa, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri anasema ni muhimu kuongeza usimamizi na kutatua changamoto za mfumo kila zinavyojitokeza.

Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kwenye Baraza la Wafanyakazi jijini Dodoma.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Amiri wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) ikifuatilia uwasilishaji wa mada hiyo. Wengine ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Ezra Kyando (kushoto) na Naibu Katibu wa Baraza la Wafanyakazi, Mhe.Christina Mlwilo (kulia).

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani (katikati) akifuatilia kwa karibu uwasilishaji wa mada hiyo. Picha chini ni sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakimsikiliza mtoa mada.



Sehemu nyingine ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi (picha mbili juu na picha mbili chini) ikimsikiliza mtoa mada.




Sehemu nyingine ya tatu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi (picha mbili juu na picha mbili chini) ikifuatilia kwa makini kinachojiri.




Sehemu nyingine ya nne ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi (picha mbili juu na picha mbili chini) ikimsikiliza mtoa mada.



Sehemu nyingine ya tano ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi (juu na picha mbili chini) ikimsikiliza mtoa mada.



Kamati Maalum ya Maazimio ya Baraza la Wafanyakazi ikimsikiliza kwa makini mtoa mada. Picha chini ni sehemu ya wajumbe wa Sekretarieti wakifuatilia kwa kina kinachojiri wakati wa mkutano wa Baraza hilo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni