Jumatano, 29 Mei 2024

MWONGOZO WA RUFAA KWA MANUSURA WA UKATILI WA KIJINSIA WAKABIDHIWA KWA WADAU KIGOMA

Na Aidan Robert, Mahakama Kigoma

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe.Rose Kangwa leo tarehe 29 Mei, 2024 amekabidhiwa Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Kigoma kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC). 

Akizungumza kwa niaba ya Wadau wote waliokabidhiwa Mwongozo huo alipokuwa akiongoza kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kigoma leo, Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Kangwa amesema, “Mwongozo huu utasaidia utoaji wa huduma za msaada wa Kisheria kwa Wadau ambao wanashughulikia manusura wa ukatili wa kijinsia ili kukuza na kusaidia wahanga kujua haki zao na katika kushughukikia upatikanaji wa haki na kufanya maamuzi sahihi kuhusu haki zao.” 

Aidha, Mfawidhi huyo amesema kuwa, Mwongozo huo umekuja muda muafaka, kwakuwa utawezesha wadau kuelewa vema jukumu lao la msingi katika kushughulikia manusura wa ukatili wa kijinsia katika maeneo yao na namna ya kuweza kuwasaidia manusara hao kulinda haki zao katika jamii husika.

Naye, Afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC), Bi. Marcela Sulley amesema, “lengo la kukabidhi Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia kwa Mkoa wa Kigoma ni kurahisisha mawasiliano kwa watoa huduma wa manusura wa ukatili wa kijinsia katika Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Kigoma.” 

Walioshiriki katika zoezi la kukabidhiwa Mwongozo huo pamoja Mahakama ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi Dawati Mkoa, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa (kulia) akipokea Kitabu cha Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia kutoka kwa Afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC), Bi. Marcela Sulley leo tarehe 29 Mei, 2024.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe.Rose Kangwa akionyesha Kitabu cha Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia  alichokabidhiwa na Afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC) kwa niaba ya Taasisi hiyo inayoshughulikia Masuala ya Ukatili wa Kijinsia katika Jamii ya Mkoa wa Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe.Rose Kangwa (aliyeketi mbele) akiongoza kikao kilichohudhuriwa na Wadau kadhau mara baada ya kukabidhiwa Kitabu cha Mwongozo wa Rufaa kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia kutoka kwa Afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC). 

Picha ya pamoja; Katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe.Rose Kangwa,  wa pili kushoto ni Afisa kutoka Shirika la Kimataifa la Uokoaji wa Jamii (IRC), Bi. Marcela Sulley, wa kwanza kushoto ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,  Bi. Edna Makala (kushoto), wa pili kulia ni Inspekta wa Polisi Dawati Mkoa wa Kigoma,  Michael Mjema na  wa kwanza kulia ni Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma, Bw. Petro Mbwanji.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni