Alhamisi, 16 Mei 2024

TUMEPANGA, TUMETEKELEZA, TUNAENDELEA KUTEKELEZA: JAJI MKUU

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wote wa Mahakama kwa kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano awamu ya pili pamoja na programu ya Maboresho ya Miaka Mitano, ambazo zinalenga pia kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Jaji Amidi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, leo tarehe 16 Mei, 2024 kwenye Baraza Kuu la Wafanyakazi linalofanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini hapa.

“Nina kila sababu ya kuwapongeza wafanyakazi wa Mahakama kutokana na kujituma kwenu kuhakikisha kuwa tunatekeleza kwa ufanisi mipango tuliyojiwekea. Tufahamu kuwa kupanga ni jambo moja na utekelezaji wa mipango ni jambo lingine, kwetu sisi tumepanga, tumetekeleza na tunaendelea kutekeleza,” amesema.

Jaji Mkuu ametoa rai kwa wafanyakazi wote kutokurudi nyuma katika jitihada za kimaboresho kwani Viongozi wa Mahakama wanatambua na kuheshimu mchango wa kila mmoja ambao ndiyo uliowezesha utekelezaji wa programu mbalimbali za kimaboresho.

Ametumia fursa hiyo kuwahimiza watumishi wote kuipokea mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania ambayo siyo tu inawalenga wananchi na watumiaji wa huduma za Mahakama kwa kuwapa huduma kwa weledi, ufanisi, uwazi na kwa haraka lakini pia inalenga kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi za utoaji wa huduma.

Jaji Mkuu ametaja mfano wa Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ambao una faida lukuki zinazolenga kurahisha utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania. 

Amesema kuwa, badala ya kupitia malundo ya majalada na karatasi kukusanya takwimu, Mfumo huu utakusanya takwimu na taarifa mbalimbali kwa njia ya elektroniki kwa usahihi. 

Jaji Mkuu amesema kuwa takwimu zitasaidia kuona yaliyojificha, hivyo kusaidia katika utekelezaji wa mipango mbalimbali na kuboresha jukumu la utoaji haki. 

“Mfumo huu utasaidia kupima utendaji wa kila mmoja wetu bila ubaguzi au uonevu kwa watumishi. Utaongeza tija, ufanisi na uono wa viwango vya utoaji wa huduma wa kila mtumiaji wa mfumo huu, kwa mfano Majaji, Wasajili, Mahakimu, Masjala za Mahakama, wadau wote wa Mahakama,” amesema.

Jaji Mkuu ametaja faida nyingine ni kupungua kwa watumishi kukutana na wadaawa uso kwa uso na kuondoa lawama za kimaadili kwa vile wadaawa na wananchi watapata fursa ya kuingia katika mfumo kutafuta taarifa bila kumuona mtumishi wa Mahakama. 

“Hakutakuwa na nafasi ya mtumishi kudhaniwa kuwa kapokea rushwa ili atoe huduma. Mfumo huu pia utaboresha usimamizi na ukaguzi. Kwa mfano, Jaji au Hakimu Mfawidhi na Wasajili, wataweza kuona kila hatua ambayo shauri lolote linapitia na kufikia mbele ya Jaji au Hakimu, bila kuliita jalada au kuomba taarifa ya mashauri kutoka kwa aliye na jalada,” amesema.

Jaji Mkuu ametaja Mfumo mwingine wa Tafsiri na Unukuzi (Transcription and Translation Software -TTS) ambao umelenga kuwapunguzia watumishi, hususan Majaji na Mahakimu, mzigo mzito wa kuandika mienendo ya mashauri kwa kalamu ya mkono. 

Ameeleza kuwa Mfumo huo unapokea sauti, uinakili hiyo sauti na kuiweka katika maandishi ya kiswahili na unao uwezo wa kutafsiri hayo maandishi kutoka lugha ya kiswahili hadi kiingereza na pia kutoka lugha ya kiingereza hadi kiswahili.

“Mfumo wa TTS tayari umefungwa na kuanza kutumika katika Mahakama 11, ikiwemo baadhi ya Mahakama Kuu (ambazo pia ni Masjala Ndogo za Mahakama ya Rufani),” Mhe. Prof. Juma amesma. 

Amesisitiza kuwa, mfumo huo wa TTS utaongeza ufanisi katika uchukuaji wa mwenendo wa shauri kwa kumpunguzia Jaji au Hakimu mzigo wa kusikiliza na kuandika kwa wakati mmoja na kuharakisha kupatikana kwa mienendo ya mashauri kwa ajili ya kukata rufani.

Jaji Amidi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi la Mahakama ya Tanzania leo tarehe 16 Mei, 2024 jijini Dodoma.

Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Mahakama ya Tanzania, Bw. Ezra Kyando akitoa utambulisho wa wajumbe kwenye Baraza hilo.

Sehemu ya wajumbe wa Baraza (juu) na Meza Kuu (chini) ikishiriki kuimba wimbo wa mshikamano kwa Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania.



Sehemu ya wajumbe wa menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (juu na picha mbili chini) wakiwa kwenye Baraza hilo.


Sehemu ya wajumbe wa Baraza (juu na picha mili chini) wakifuatilia kinachojiri.



 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni