Na Mwandishi wetu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda
ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewahimiza wadau wa haki wanaoshiriki mafunzo ya
namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori na makosa
ya misitu kuzingatia vema sheria, kanuni na taratibu ili kuondoa changamoto
zinazojitokeza katika hatua mbalimbali za uendeshaji wa mashauri hayo.
Mhe. Jaji Mtulya ametoa kauli hiyo tarehe
13/05/2024 wakati akifungua
mafunzo hayo ya awamu ya tano ya wadau wa haki jinai zaidi
ya 179 katika ukumbi wa Blue Sky Hotel mjini Tarime mkoani Mara ambayo
yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya PAMS
Foundation inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na
usalama wa Wanyamapori.
Mafunzo hayo yatakayodumu kwa wiki moja hadi tarehe
17/05/2024 yanawajumuisha washiriki ambao ni Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu,
Waendesha Mashtaka na Wapelelezi wa
ngazi mbalimbali kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Simiyu na Mara.
Katika hotuba yake, Mhe. Jaji Mtulya amesema: “Mashauri
haya ya wanyamapori yana sheria zake, kuna taratibu nyingi kuanzia mtu
anapokamatwa mpaka mtu kuhukumiwa, ila taratibu hizo mara nyingi huwa
zinakosewa na wadau, hivyo tunakutana hapa ili kupeana ufahamu wa pamoja katika
kutatua changamoto hizo ili tuweze kulinda rasilimali hizo na kulinda uchumi wa nchi.”
Nae Mkurugenzi wa mafunzo ya Kimahakama kutoka Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Dkt. Patricia Kisinda amesema kuwa
mafunzo hayo yameandaliwa baada ya utafiti uliyofanywa na IJA kubaini uwepo wa
kasoro katika kuendesha mashauri hayo ya uhalifu dhidi ya wanyamapori na makosa
ya misitu.
Kuhusu matarajio baada ya mafunzo hayo, Mhe. Dkt
Kisinda amebainisha: “Matarajio yetu ni kwamba washiriki hawa watakaporudi
katika vituo vyao vya kazi ni kuweza kuyaweka katika vitendo yale
waliyofundishwa darasani, kwa sababu katika mafunzo haya wanafundishwa kwa
vitendo ikiwemo kupelekwa mbugani kuona kwa vitendo yale waliyofundishwa
darasani ambayo yanahusiana na rasilimali hizo za wanyamapori na misitu.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa
PAMS Foundation, Bw. Samson Kassala amewaambia washiriki hao kuwa wana jukumu
kubwa katika mapambano dhidi ya majangili na kulinda rasilimali hizo muhimu kwa
taifa.
“Ni muhimu mkatambua kuwa mna jukumu zito katika
mapambano ya kitaifa dhidi ya majangili. Kujitoa kwenu na ustahimilivu wenu
ndio msingi wa matumaini ya Tanzania katika kulinda mali hizo,” amesema Bw.
Kassala.
Nae mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Afisa
muhifadhi kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA), Gift
Sanga amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia ufahamu wa kutatua changamoto
zinazojitokeza katika hatua mbalimbali hususani za ukamataji na uchukuaji wa
vielelezo vya ushahidi.
“Kumekuwepo na changamoto katika hatua za mwanzo za
ukamataji, kwani kuna baadhi ya ukamataji unakuwa haujafuata sheria pamoja na
uchukuaji wa kielelezo pamoja na kukihifadhi. Hivyo kukosewa kwa hatua hizo
kunasababisha changamoto katika kuendesha mashauri,” amesema Bw. Sanga.
Mafunzo hayo
ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya IJA na PAMS Foundation na
yameshafanyika katika mikoa zaidi ya 20 huku washiriki 785 wakinufaika na
mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa awamu ya mwisho hapa Tarime.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akihutubia wakati wa ufunguzi wa mafunzo yahusuyo namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori na makosa ya misitu wilayani Tarime mkoani Mara tarehe 13/05/2024.
Mkurugenzi wa mafunzo ya Kimahakama kutoka Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akitoa neno la
utangulizi wakati wa ufunguzi wa mafunzo yahusuyo namna bora
ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori
na makosa ya misitu wilayani Tarime mkoani Mara.
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo
yahusuyo
namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori
na makosa ya misitu wakimsikiliza mgeni rasmi ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu
Mtulya(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo yahusuyo namna bora
ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori
na makosa ya misitu wilayani Tarime mkoani Mara.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa PAMS Foundation
Bw. Samson Kassala akihojiwa na vyombo vya habari wakati
wa ufunguzi wa mafunzo yahusuyo namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori na
makosa ya misitu wilayani Tarime mkoani Mara.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo yahusuyo namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori na makosa ya misitu wilayani Tarime mkoani Mara.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu
Mtulya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo yahusuyo
namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori
na makosa ya misitu wilayani Tarime mkoani Mara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni