Alhamisi, 16 Mei 2024

MAHAKAMA YAVUKA LENGO MUDA WA WASTANI USIKILIZAJI MASHAURI

§  Mlundikano wa mashauri waendelea kupukutika

§  Malalamiko kwenye mirathi, dhamana yapungua 

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Muda wa wastani unaotumika kumaliza shauri umeshuka kutoka siku 95 mwaka 2022 hadi 84 mwaka 2023, huku Mahakama katika ngazi zote zikivuka lengo la wastani wa muda wa kusikiliza shauri.

Mfanikio hayo yamebainishwa leo tarehe 16 Mei, 2024 na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya alipokuwa anawasilisha taarifa yake kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi linalofanyika Jijini Dodoma.

Msajili Mkuu amebainisha pia kuwa, mlundikano wa mashauri umeshuka toka asilimia sita hadi asilimia tano kwa mwaka 2023 na umeendelea kushuka hadi asilimia nne mwezi Aprili, 2024

Ameeleza kuwa Mahakama ilifanya vikao maalumu vya kuondoa na kuzuia mlundikano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama isipokuwa Mahakama za Mwanzo. 

“Kwa Mahakama Kuu na Mahakama za chini, yaani Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya, mashauri 1,700 yalipangwa na 1,393, sawa na asilimia 82, yalimalizika,” amesema.

Mwishoni mwaka 2023, idadi ya mashauri ya mlundikano ilikuwa 2,594, sawa na asilimia tano ya mashauri 51,330 yaliyokuwa yakiendelea katika ngazi zote za Mahakama. 

Kwa kulinganisha na mwaka 2022, iliyokuwa na mlundikano wa asilimia sita, mwaka 2023 mlundikano ulipungua kwa asilimia moja ukizingatia kuwa usajili wa mashauri uliongezeka kwa asilimia tatu katika mwaka 2023 kutokana na mafanikio ya usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao.

Mhe. Nkya ameeleza kuwa utandaji mzuri wa watumishi wa Mahakama, wakiwemo Majaji na Mahakimu, umesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa malalamiko ya wananchi na kuongeza imani katika utoaji haki kutoka asilimia 78 mwaka 2019 hadi asilimai 88 mwaka 2023.

Amebainisha maeneo yanayolalamikiwa zaidi au mara kwa mara, ikiwemo mashauri ya mirathi kuhusu kutokuhitimishwa kwa wakati, malipo ya fedha za mirathi, wasimamizi wa mirathi kuhodhi mali za marehemu.

Eneo jingine ambalo malalamiko yamepungua ni utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama kuchukua muda mrefu na urejeshwaji wa fedha iliyolipwa kwenye akaunti ya Mahakama kama faini au dhamana kuchelewa kurejeshwa pale shauri inapohitimishwa.

Maeneo mengine ni malalamiko ya upatikanaji wa nakala za hukumu na mwenendo wa mashauri, utoaji wa hati za kimahakama, dhamana, muda wa kuanza shughuli za kimahakama na maadili ya Maafisa wa Mahakama.

Kwa upande wa Mahakama Inayotembea, Msajili Mkuu amebainisha kuwa mwaka 2023 mashauri 1,151 yalisajiliwa na mashauri 1,264, sawa na asilimia 110 yalimalizika.

Mhe. Nkya ameeleza kuwa kati ya Januari-Aprili, 2024, mashauri 778 yamesajiliwa na 764, sawa na asilimia 98 yamemalizika, huku mashauri 53 yakiwa yanaendelea.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (juu na chini) akiwasilisha taarifa yake kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi linalofanyika Jijini Dodoma leo tarehe 16 Mei, 2024.


Sehemu ya wajumbe wa  Baraza la Wafanyakazi (juu na chini) wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri kwenye mkutano wao.


Sehemu nyingine ya wajumbe wa  Baraza la Wafanyakazi (juu na chini) wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri kwenye mkutano wao.


Sehemu nyingine ya tatu ya wajumbe wa  Baraza la Wafanyakazi (juu na picha mbili chini) wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri kwenye mkutano wao.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni