Na Mwandishi Wetu
Watumishi pamoja na Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wamemuaga mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo hicho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald
Ndika baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka sita ya kulitumikia
Baraza hilo.
Hafla ya kumuaga Mhe. Dkt. Ndika imefanyika tarehe
13/05/2024 katika ukumbi wa mafunzo wa Ibrahim Hamis Juma hapa Chuoni Lushoto
mkoani Tanga.
Mhe. Dkt. Ndika aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Marehemu Dkt John Magufuli tarehe 17/06/2018 kushika wadhifa huo
akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe.
John Mrosso ambae alikuwa amemaliza muda wake wa kulitumikia Baraza hilo kwa
kipindi cha miaka sita.
Watumishi wa IJA pamoja na Wajumbe hao wa Baraza
walimuaga Mwenyekiti huyo kwa kumpatia zawadi mbalimbali zikiwemo za
tarakilishi mpakato (laptop) na tuzo maalumu ikiwa ni kuuenzi mchango wake
katika kulitumikia Baraza hilo la Uongozi wa Chuo kwa mafanikio makubwa.
Katika nasaha zake, Mhe. Dkt. Ndika amesema kuwa ni
fahari kubwa kwake kuliongoza Baraza hilo na kwamba mafanikio yaliyopatikana
chini ya Uongozi wake ni ya watu wote wakiwemo watumishi pamoja na wajumbe wa
Baraza.
Aidha, amesema kuwa katika kipindi chake, Chuo kimepiga
hatua katika kuendesha mafunzo ya Kimahakama, kufanya utafiti na kutoa ushauri
elekezi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa
Mahakama ya Rufani na Katibu wa Baraza hilo Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo
amebainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Mhe. Jaji
Ndika kuwa ni mabadiliko ya sheria ya Chuo ya mwaka 1998 yaliyofanyika mwaka
jana ambayo yanampa mamlaka mbalimbali Jaji Mkuu wa Tanzania ikiwemo kuteua
wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo pamoja na Muundo mpya wa Uongozi wa Chuo
ambao umeanzisha Kurugenzi ya Mafunzo ya Kimahakama ikiwa ni mara ya kwanza
tangu Chuo hicho kianzishwe zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt.
Gerald Ndika akionesha zawadi aliyopatiwa na Watumishi wa pamoja na Wajumbe wa
Baraza la Uongozi IJA baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka sita ya
kulitumikia Baraza hilo.
Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Katibu
wa Baraza hilo Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akimkabidhi tuzo maalumu Mwenyekiti wa
Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye
pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika Chuo baada ya kumaliza
kipindi chake cha miaka sita ya kulitumikia Baraza hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt.
Gerald Ndika akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti
na wa Baraza la Chuo.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika akiwa anaonyesha zawadi ya tarakilishi mpakato (laptop) aliyokabidhiwa na watumishi wa IJA na tuzo maalumu ikiwa ni kuuenzi mchango wake katika kulitumikia Baraza hilo la Uongozi wa Chuo kwa mafanikio makubwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni