Ijumaa, 21 Juni 2024

MTENDAJI MKUU ATETA NA WATUMISHI WA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA

Na LIGHTNESS EURENUS KABAJU-Mahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 20 Juni, 2024 alitembelea Kituo cha Huduma kwa Mteja kilichopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni jijini Dar es Salaam na kufanya kikao na watumishi wa kituo hicho.

Akiwa katika Kituo hicho, Mtendaji Mkuu alipokea taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Denice Domician Mlashani, ambaye pia ni Mtalaam wa kuchakata na kupitia mrejesho wa wananchi wa Kituo hicho.

Katika taarifa yake, Mhe. Mlashani amemweleza Mtendaji Mkuu kuhusu mrejesho wa Kituo hicho kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake mnamo tarehe 01 Machi, 2022.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba Kituo hufanya kazi kwa kupokea mirejesho ambayo ni malalamiko, maoni au mapendekezo, maulizo na pongezi kutoka kwa wananchi kwa kupitia namba ya simu ambapo mteja ataweza kuwasiliana na mtoa huduma moja kwa moja, yaani kupiga simu au kutuma ujumbe   kupitia namba 0752 500 400 na 0739 502 401. 

Alibainisha pia kuwa mwananchi anaweza kuwasiliana na Kituo kupitia barua pepe ambayo ni maoni@judiciary.go.tz. Aidha, Mhe. Mlashani alieleza uwepo wa namba ya simu ya kupiga bure ambayo ni +255 800 750 247.

Taarifa hiyo pia imeonesha mwenendo wa mirejesho inavyoshughulikiwa kwa ufanisi na kwa wakati, hivyo kufanya Kituo kuwa nyenzo muhimu katika Mahakama ya Tanzania. 

Alisema malalamiko kutoka kwa wananchi yamepungua kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri, utoaji wa hati za kimahakama, dhamana, muda wa kuanza shughuli za kimahakama na maadili juu ya maafisa wa Mahakama.

Vilevile, Mhe. Mlashani alieleza kuwa wananchi wameendelea kutoa maoni chanya ya kuweza kuboresha huduma kwa wateja ambapo baadhi ya maoni hayo ni urejeshwaji wa mashauri ya ardhi katika Mahakama za kawaida, kuongeza Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, kuongezwa idadi ya Mahakimu, hasa katika Mahakama za Mwanzo na kuficha utambulisho wa wadaawa katika mashauri ya talaka na ndoa.

Naye Bi. Evetha Evarist Mboya, ambaye ni Afisa Utumishi na Msimamizi katika Kituo hicho alieleza mafanikio ya ambayo ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa kushughulikia mirejesho kwa njia rahisi na ya kisasa ambapo mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika mara baada ya kukamilika. 

Alitaja mafanikio mengine kama kutembelea Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki na kutoa elimu, lakini pia kutembelea magereza na kupata mirejesho kutoka kwa wafungwa.

Mtandaji Mkuu amewapongeza watumishi katika Kituo hicho kwani huduma hiyo ni nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama inayolenga ushirikishwaji wa wadau na kurejesha imani kwa wananchi juu ya huduma zinazotolewa na mahakama. 

Vilevile amewapa elimu adhimu ya namna bora ya kuwasiliana na wananchi pindi wanapohitaji huduma kupitia kituo hicho. Prof. Ole Gabriel alitumia fursa hiyo kuwaasa watumishi hao kufanya kazi kwa weledi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (juu na chini) akizungumza na watumishi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja baada ya kuwatembelea jana tarehe 20 Juni, 2024. 


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel  akimsikiliza mmoja wa watumishi hao.


Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami akizungumza wakati wa kikao hicho.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi hao (juu na chini).


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni