• Ipo mbioni kutoa Toleo la kwanza la maamuzi ya Januari-Juni, 2024
Na ARAPHA RUSHEKE na TAWAN SALUM, Mahakama-Dodoma
Bodi ya Jaji Mkuu ya Juzuu la Taarifa za Sheria Tanzania ipo katika kikao cha siku tatu cha uchambuzi wa maamuzi ya mwaka 2024 kwa ajili ya kutoa Kitabu cha Toleo la kwanza (Volume 1) kwa maamuzi ya Mwezi Januari hadi Juni mwaka huu.
Akizungumza jana tarehe 29 Julai, 2024 wakati akifungua kikao hicho kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Midland jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jacobs Mwambegele alisema Kikao hicho ni cha mara ya pili kufanyika kwa mwaka huu.
“Bodi inakutana ikiwa tayari imekwishaandaa Taarifa ya Juzuu la Sheria Tanzania la Mwaka 2021 hadi Mwaka 2023. Ikiwa vyote vipo kwa Mzabuni katika hatua ya uchapaji na katika kikao hiki Bodi itakamilisha Taarifa ya Juzuu la Sheria Kitabu cha kwanza Toleo la kwanza kwa Mwaka (Volume 2),” alisema Mhe. Mwambegele.
Mhe. Mwambegele aligusia pia kuanza kutumika kwa Juzuu la Sheria la Mwaka 2007 hadi Mwaka 2021 katika mfumo wa nakala laini (Online Law Reports 2007/2021) hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu ili kuweza kuwafikia watumiaji wengi kwa kuwa machapisho ya nakala ngumu ni gharama na hayawafikii wengi.
Aliongeza kuwa, katika kikao kijacho Bodi hiyo itaendelea na Taarifa ya Juzuu la Sheria kwa Mwaka 2024 Toleo la pili (Volume 2), lengo likiwa ni kutoa kitabu cha Juzuu la Sheria kila baada ya robo mwaka kwa kipindi kijacho.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mratibu wa Bodi, Mhe. Kifungu Kariho alisema kwamba, upatikanaji wa maamuzi katika Bodi umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwakuwa maamuzi mengi yanapatikana kwenye Mfumo wa Mahakama unaochapisha Maamuzi, Sheria na Kanuni bure mtandaoni (TanzLII).
“Kwa kipindi kijacho cha miaka miwili, zoezi hili litarahisishwa zaidi baada ya muunganiko wa Mfumo wa Kielektroniki wa Mashauri wa Mahakama, Maktaba Mtandao pamoja na Mfumo wa TanzLII na kuongeza kasi ya kuchambua maamuzi hayo. Lengo la Bodi ni kutoa Kitabu cha Juzuu la Sheria mara nne kwa mwaka, yaani kila baada ya robo mwaka,” alisema Mhe. Kariho.
Bodi hiyo inachambua maamuzi ya Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Bodi hiyo ina wajumbe 11, ambao ni Majaji kutoka Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahkama Kuu ya Zanzibar, Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoka Bara na Zanzibar na Wawakilishi wa Vyama vya Mawakili Tanzania Bara na Zanzibar.
Wajumbe wa Bodi ya Jaji Mkuu ya Juzuu la Taarifa za Sheria Tanzania wakiwa katika kikao hicho. Kushoto ni Hassan Haji na kulia ni Bi. Nelly Mwasongwe.
Sehemu ya wajumbe wa kikao wakifuatilia kinachojiri katika kikao hicho.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni