Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo jana terehe 30 Julai, 2024 alifanya ziara ya Mahakama mkoani hapa kukagua shughuli mbalimbali za kiutendaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Dodoma.
Akiwa katika Mahakama hizo zilizopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, Mhe. Dkt. Massabo alipokea taarifa za usikilizaji wa mashauri na masuala ya utawala na kupongeza kazi kubwa inazofanywa na watumishi.
Hata hivyo, Jaji Mfawidhi alitumia fursa hisyo kusisitiza mambo mbalimblai, ikiwemo uadilifu, weledi na uwajibikaji.
“Kufanya kazi kwa bidii na uadilifu sio ombi ni sheria, uadilifu ni pamoja na kutunza siri, kuwa na mienendo mizuri kwenye kazi na hata nje ya kazi, pamoja na kujiepusha na vishawishi vya rushwa…
“…uadilifu hauangalii changamoto ulizonazo, tusiache kabisa kuwa waadilifu sisi tupo makao makuu ya Nchi, ni kioo cha kila jambo. Tutimize majukumu yetu kikamilifu,” alisema Mhe. Dkt. Massabo.
Kadhalika alisisitiza utoaji wa huduma bora na nzuri eneo la kazi, kuendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wadau kwenye masuala mbalimbali ya sheria muda wa asubuhi kabla ya kuanza ratiba za Mahakama.
Jaji Mfawidhi pia alihimiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na watumishi kuendelea kupewa elimu juu ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa Mwaka 2020/2021-2024/2025.
Sambamba na hayo, aliwakumbusha watumishi kuendelea kutekeleza maelekezo mbalimbali ya Viongozi, likiwemo utoaji nakala za hukumu siku hiyo hiyo baada ya kusomwa.
Viongozi wengine waliokuwapo katika ziara hiyo ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe Upendo Ngitiri, Mtendaji wa Mahakama, Bw. Sumera Manoti, Mahakimu Wafawidhi Mahakama hizo pamoja na watumishi wengine.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni