Alhamisi, 25 Julai 2024

KITUO CHA MASUALA YA FAMILIA TEMEKE CHAKUTANA NA WADAU

Waja na Mpango wa Kumaliza Mashauri ya Mlundikano.

Kituo kimedhamiria kutoa elimu kwa Wadau walio karibu na wananchi.

Changamoto za mashauri ya Mirathi zabainishwa na kuwekewa mikakati

Na Naomi Kitonka, Kituo Jumuishi cha Masuala Ya Ndoa na Familia- Temeke

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Ndoa na Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa jana tarehe 24 Julai, 2024 aliwaongoza Mahakimu na wadau mbalimbali wa Mahakama katika kikao cha Kamati ya kusukuma Mashauri ya Madai (Bench Bar Meeting) kuwawezesha kupitia mashauri ya mlundikano kwa pamoja na kuona namna bora ya usikilizwaji wa haraka pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuyamaliza mashauri hayo.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho kilichofanyikia katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho, Mhe. Mnyukwa alizungumzia juu ya umuhimu wa kikao hicho kwa wajumbe ambao ni wadau wa Mahakama kutoka katika Taasisi mbalimbali na mchango wao mkubwa katika kusukuma mashauri ya mlundikano katika Mahakama.

“Tunawashukuru wadau wetu kwa kuitikia wito wetu katika kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa kusukuma Mashauri ya madai na kama Mahakama ya Kituo Jumuishi Temeke tunatambua mchango wenu mkubwa katika upatikanaji wa haki kwa wananchi pamoja na nafasi kubwa ya kusaidia kuwaelimisha wananchi na kuongeza uelewa wao katika zoezi zima la upatikanaji wa haki kwa kujua mambo muhimu hasa katika mashauri ya madai,” alisema Jaji Mnyukwa.

Pamoja na hayo wadau walipata wasilisho kutoka kwa Katibu wa kikao ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Frank Moshi ambaye alitoa takwimu za hali ya mashauri kutoka Mahakama Kuu, Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo paoja na sababu zilizochangia kutokumalizika kwa wakati katika Mahakama zote katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka.

Kadhalika, Wadau nao walipata nafasi ya kutoa maoni yao baada ya wasilisho, walieleza kwamba, changamoto kubwa ni kuwa na muda mrefu wa kufuatilia mashauri ya mirathi pamoja na kuchelewa kufunga mirathi kwa wakati.

Kuhusu changamoto hiyo,  Jaji Mfawidhi alijibu kwa kusema, “changamoto hiyo inatokana na wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu taratibu sahihi za kufuata wanaposhughulikia masuala ya mirathi, lakini pia ukosefu wa elimu kwa wadau inachangia wao kutokutoa taarifa muhimu na msaada wa kutosha hivyo kuchangia ukwamishaji wa zoezi la kusukuma mashauri na upatikanaji wa haki kwa wakati.”

Aliongeza kuwa, lengo la Kituo hicho ni kuhakikisha mashauri yote katika kila ngazi ya Mahakama yanamalizika kwa muda husika na kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wengine.

Alisema pamoja na kuwa na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yaliyoibua changamoto mpya, Mahakama kama Taasisi imekuwa makini katika kuzipatia ufumbuzi na kutoathiri kasi ya uondoshwaji wa mashauri na changamoto zimetumika kama fursa ya kuonesha weledi katika utendaji na kuhakikisha huduma za uhakika zinapatikana kwa wananchi kwa wakati.

Vilevile, Jaji Mfawidhi huyo alieleza kuwa, kama Mahakama ya Kituo Jumuishi Temeke imekusudia kuwa na hatua na mpango wa vikao vya usikilizwaji  mashauri vya mara kwa mara.

Aidha, kikao hicho kilitoka na maazimio ili kuhakikisha wateja wanafutwa machozi kama kauli mbiu ya Kituo hicho inavyosema ‘kutoa haki kwa wanachi kwa muda unaotakiwa na kuongeza ufanisi wa kituo katika ngazi zote za utendaji’.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mtendaji wa Kituo, Bw. Samson Mashalla, Naibu Wasajili, Mhe. Frank Moshi na Mhe. Evodia Kyaruzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya-Temeke, Mhe. John Msafiri, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo-Temeke, Mhe. Aloyce Mwageni akiambatana na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Watoto, Mhe. Orupa Solomon Mtae.

Pamoja na hao, Wadau waliohudhuria kikao hicho ni kutoka PSSSF, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hati, Maafisa Ustawi wa Jamii, Mwakilishi kutoka Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) pamoja na Watoa Msaada wa Kisheria  (WiLDAF, WLAC) waliopo katika Kituo Jumuishi Temeke.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (kushoto) akiwa kwenye kikao  cha Kamati ya kusukuma Mashauri ya Madai (Bench Bar Meeting)  kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho jana tarehe 24 Julai, 2024. Kulia ni Jaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Sharmillah Sarwatt. 

Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai ambao ni wadau wa Mahakama kutoka Taasisi mbalimbali wakisikiliza kwa makini kinachojiri katika kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 24 Julai, 2024 IJC Temeke.

Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (hayupo katika picha). Kikao hicho kilifanyika jana tarehe 24 Julai, 2024. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya-Temeke, Mhe. John Msafiri (aliyesimama) akichangia mada katika katika kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika jana tarehe 24 Julai 2024 IJC Temeke.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni