Na Innocent Kansha-Mahakama, Njombe
Mahakama
mkoani Njombe ilivuka mwaka 2023 ikiwa na mashauri sifuri ya mlundikano na kufikia
Disemba 2023, mashauri yaliyobaki yalikuwa 522 na hivyo kufikia lengo la
kuondosha mashauri ya muda mrefu mahakamani.
Akiongea
na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania
leo tarehe 23 Julai, 2024 Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe Bw.
Richard Mbambe amesema, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilibakiwa na mashauri 19
Disemba, 2023, huku Mahakama za Wilaya zilibakiwa na mashauri 207 na Mahakama
za Mwanzo mashauri 296.
“Mahauri
yaliyofunguliwa kuanzia Januari 2024 hadi Juni 2024 Mahakama ya Hakimu Mkazi ilipokea
mashauri 27, Mahakama za Wilaya mashauri 201 na Mahakama za Mwanzo mashauri
1132 takimu hizo zinafanya jumla ya mashauri yamefikia takribani 1360,” amesema
Mtendaji Bw. Mbambe.
Bw.
Mbambe amesema, mashauri yaliyosikilizwa kunzia Januari, 2024 hadi Juni, 2024
Mahakama ya Hakimu Mkazi imesikiliza mashauri 30, wakati Mahakama za Wilaya
zimesikiliza mashauri 348 na Mahakama za Mwanzo zimesikiliza mashauri 900 na
kufanya jumla ya mashauri 1278.
Mashauri
yaliyobakia kufikia Juni, 2024 kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ni
mashauri 16, Mahakama za Wilaya ni mashauri 60 na Mahakama za Mwanzo ni
mashauri 528 na kufanya jumla ya mashauri yaliyobaki kufikia 604, amesema
Mtendaji huyo.
Kwa
upande wa mashauri yaliyoendeshwa kwa njia ya Mahakama Mtandao (video
Conference) ni mashauri 12 kunzia Januari hadi Juni, 2024 mashauri
yaliyosikilizwa Mahakama ya Hakimu Njombe ambayo hayakusajili wa Njombe ni mashauri
manne (4) kutoka Mtwara shauri moja (1), Kigoma moja (1) na Iringa mashauri mawili
(2) hii inatokana na uimarishaji wa matumizi ya mifumo ya kuendeshea mashauri
kwa njia ya mtandao.
Bw.
Mbambe amesema, Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe hupokea wastani wa wateja 668
kwa mwezi, ikiwa ni sawa na wastani wa wateja 167 kwa wiki wanaofika mahakamani
hapo kupata huduma mbalimbali za utoaji haki. Vilevile malalamiko
yaliyowasilishwa na wateja kwa mwaka 2023 yalikuwa saba (7) na Mwaka 2024 kuanzia
Januari hadi Juni 2024 Mahakama imepokea malalamiko mawili (2) na tayari uongozi
umeshayashughulikiwa.
Akielezea maendeleo ya miradi ya ujenzi
inayotekelezwa mkoani Njombe na Mahakama ya Tanzania, Bw. Mbambe amesema
Mahakama kwa sasa inatekeleza miradi miradi mitatu (3) ya ujenzi, ikiwemo
ujenzi wa Mahakama Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Njombe ambao ujenzi wake umefikia asilimia 21, ujenzi wa Mahakama
ya Mwanzo Lupembe na Mahakama ya Mwanzo Manda.
Ujenzi
wa Kituo Jumuishi Njombe ulianza tarehe 12 Disemba, 2023 na unatarajiwa
kukamilika tarehe 11 September, 2024. Mradi huu unatarajiwa kugharimu Tshs.
7,647,179,528.62/= (VAT). Mkandarasi anayejenga mradi huu ni Shandon Hi – Speed
Dejian Group chini ya usimamiziwa mkandarasi Mshauri (Consultant) Crystal
Consultant.
Aidha,
mradi upo katika hatua ya ukamilishaji wa sakafu ya ghorofa ya kwanza (first
floor slab concrete) hivyo kufanya asilimia ya utekelezaji wa mradi kuwa asilimia
21.
Mtendaji
huyo ameongeza kuwa, mradi huo ukikamilika utasaidia kusogeza
huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi badala ya kusafiri kufuata
huduma za Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa kama ilivyo sasa, pia itapunguza
gharama za kuleta Waheshimiwa Majaji toka Mahakama Kuu vilevile itapunguza
mlundikano wa mshauri, itawasaidia wananchi kutumia muda wao katika uzalishaji
mali na kujiongezea kipato na kurahisiha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Kwa
mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Mkoa wa Njombe una idadi ya
wakazi wapatao 889,946 ambao watanufaika na ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki kitakapo kamilika na kuanza kutumika kutoa huduma za haki mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa takwimu Mkoa wa Njombe una Mahakama ya Hakimu Mkazi 1, Mahakama za Wilaya nne (4) na Mahakama za Mwanzo 26 kama inavyobainishwa hapo chini.
Wilaya ya Njombe ina Mahakama moja ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo saba (7), ambazo ni Njombe mjini, Makambako, Lupembe, Matola, Igominyi, Mtwango na Uwemba/Mahenye.
Wilaya ya Ludewa inayo Mahakama ya Wilaya moja na Mahakama za Mwanzo saba (7), ambazo ni Ludewa mjini, Mlangali, Mawengi, Lugarawa, Mavanga na Manda/Masasi na Luilo.
Wilaya
ya Makete ina Mahakama ya Wilaya moja ambayo mashauri yake hufanyika katika
jengo la Mahakama ya Mwanzo Makete mjini. Aidha, kuna Mahakama za Mwanzo nane (8)
ambazo ni Makete mjini, Bulongwa, Matamba, Lupalilo, Lupila, Ukwama, Mfumbi na
Ipelele.
Wilaya
ya Wanging’ombe ina Mahakama ya Wilaya moja, aidha Wilaya ya Wanging’ombe inazo
Mahakama nne (4) za Mwanzo ambazo ni Wanging’ombe, Mdandu, Kipengere na
Imalinyi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni