- Yafanya maamuzi ya mashauri kwa kiwango
cha asilimia 93.3 cha mashauri yaliyopangwa.
- ·Changamoto za Mawakili zapatiwa ufumbuzi.
Vikao vya Mahakama ya Rufani ya Tanzania vilivyojumusha majopo mawili yenye jumla ya Majaji wa Mahakama ya Rufani saba (7) vimehitimishwa jijini Mwanza ambapo jumla ya mashauri 70 yamesikilizwa na kutolewa uamuzi kati ya mashauri 75 yaliyokuwa yamepangwa.
Akitoa taarifa ya mashauri na mwenendo wa vikao hivyo vilivyoanza kusikilizwa tarehe Mosi Julai, 2024 na kuhitimishwa leo tarehe 19 Julai, 2024 Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Daines Lyimo amesema kuwa, jumla ya mashauri 5 sawa na asilimia 6.7 ndiyo yameahirishwa kutokana na sababu mbalimbali kati ya mashauri 75 yaliyopangwa katika vikao hivyo.
“Katika vikao hivi ambavyo vilikuwa na majopo mawili, Mwenyekiti wa Jopo A alikuwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Frednand Leons Katipwa Wambali, na Mwenyekiti wa Jopo B liliongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Lugano Samson Mwandambo, majopo yote yamesikiliza na kuamua jumla ya mashauri 70 sawa na asilimia 93…
…Mhe. Lyimo amesema, mashauri yaliyosikilizwa na kutolewa uamuzi ni mashauri 48 na mashauri 22 yanasubiri kutolewa uamuzi wakati wowote kuanzia sasa” amesema Mhe. Lyimo.
Katika vikao hivyo kulikuwa na mashauri ya rufaa za jinai 22 na zote zimesikilizwa na kutolewa uamuzi. Wakati rufaa za madai zilipangwa 22 na kati ya hizo 20 zimesikilizwa na mbili (2) zimeahirishwa kutokana na sababu za marekebisho ya vitabu vya kumbukumbu za rufaa husika pamoja na uhitaji wa Mfilisi kuingizwa kwenye mashauri. Maombi ya madai yaliyopagwa yalikuwa mashauri 31 kati ya hayo mashauri 28 yamesikilizwa na kutolewa uamuzi na yaliyoahirishwa ni mashauri 3.
Mhe. Lyimo amesema, ujumla ya mashauri 5,034 yameandikishwa kusikilizwa na Mahakama ya Rufani ya Tanzania hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2024 katika Masjala zote Tanzania huku Masjala ya Dar es Salaam ikiwa na mashauri 2,269 sawa na asilimia 45.07 na masjala ya Morogoro ikiwa na mashauri 30 sawa na asilimia 0.6.
Aidha,
akizungumza kwa niaba ya Mawakili walikuwa wakiwawakilisha warufani katika
vikao hivyo, wakili Kassim Gilla aliushukuru uongozi wa Mahakama Kanda ya
Mwanza kwa kuweza kuzifanyia kazi changamoto ambazo mawakili walikuwa
wanazipitia wakati walipohitaji kuonana na warufani waliopo gerezani. Kwani
hapo awali walikuwa wanachukuwa muda mrefu kuonana na warufani. Lakini kwa sasa
hiyo changamoto haipo tena na wanaonana na wahusika kwa wakati.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Paul
Kihwelo akiongea jambo na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Benhajj Masoud wakati wa kikao cha tathmini ya mashauri ya Rufaa kilichofanyika tarehe 19
Julai 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza.
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria kikao cha tathmini ya mashauri ya Rufaa kilichofanyika tarehe 19 Julai 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza wakifuatilia kwa makini kinachozungumzwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Frednand Wambali (wa kwanza kushoto) na Mwenyekiti wa kikao hicho.
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria kikao cha tathmini ya mashauri ya Mahakama ya Rufani kilichofanyika tarehe 19 Julai 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza wakifuatilia kwa makini kinachozungumzwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Frednand Wambali (aliyenyoosha kidole) na akiwa Mwenyekiti wa kikao hicho akifafanua jambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni