Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Zanzibar
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amesema kuwa uimarishaji wa mfumo wa utoaji haki nchini huweka mazingira bora yenye kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi.
Mhe. Siyani ameyasema hayo leo tarehe 19 Julai, 2024 alipokuwa anazungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Kikao Kazi baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi kinachofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort.
“Sote tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali zote mbili kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi. Imani ya wawekezaji haiwezi kukamilika kama mfumo wa utoaji haki haujaimarishwa,” amesema.
Jaji Kiongozi amebainisha kuwa wawekezaji wanataka kuhakikishiwa kuwa kuna mfumo wa kutoa haki utakaolinda maslahi ya Waajiri na Waajiriwa.
Amesema kuwa vikao vya kujengeana uwezo kama hicho ni muhimu kwani Majaji na Wadau wengine wa haki kazi huweza kutoa huduma ya uhakika na haraka, hivyo kuongeza imani kwa wananchi.
Mhe. Siyani amewaambia washiriki wa Kikao Kazi hicho kutumia jukwaa hilo kuhamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za kimahakama.
Jaji Kiongozi amebainisha kuwa ni wazi katika zama hizi, matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma yoyote hayakwepeki na Taasisi yoyote itakayobaki nyuma haitaweza kushindana.
“Kwa hiyo, kupitia majadiliano, washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu jinsi TEHAMA, kama moja ya nyenzo muhimu ya utoaji haki, inavyoweza kurahisisha upatikanaji wa haki na kutafakari namna mifumo ya Mahakama, mifuko ya hifadhi ya jamii na mifuko ya fidia kwa wafanyakazi inavyoweza kusoma na kuongeza tija,” amesema.
Mhe. Siyani ameeleza pia kuwa kwa kutambua uwepo wa changamoto zinazojidhihirisha kupitia maamuzi mbalimbali kwenye eneo hilo, Mahakama ya Tanzania, hususan Divisheni ya Kazi na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi iliona ni vema wadau wa haki kazi wakapata nafasi ya kukutana, kujadiliana na kubadilishana uzoefu utakaoongeza ujuzi na kuboresha utendaji kazi.
Kadhalika, Jaji Kiongozi ameeleza kuwa kufanyika kwa Kikao Kazi hicho Zanzibar kumeleta sura ya kipekee ya kudumisha Muungano kwa kuwaleta pamoja washiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema kuwa jukwaa hilo linawapa fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu Sheria za Kazi, Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazai na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, hivyo kuboresha uwezo wa utatuzi wa migogoro katika maeneo ya kazi.
“Kufanyika kwa mafunzo haya ni mwendelezo wa jitihada za kufanikisha utekelezaji wa Nguzo ya Pili na ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama juu ya upatikanaji haki kwa wakati na ushirikishwaji wa wadau,” Mhe. Siyani amesema.
Ameelezea matumaini yake kuwa maarifa na ujuzi utakaopatikana kuptia kikao kazi hicho yatasaidia washiriki katika utatuzi wa migogoro ya kazi.
Mhe. Siyani ametumia fursa hiyo kuishukuru Menejimenti ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa namna ambavyo wameendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa kukubali kuendelea kuwezesha vikao kazi mbalimbali vya namna hiyo na kutoa fursa kwa Majaji, Maafisa na Wadau wa haki kazi kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.
Amekumbusha kuwa kikao kazi cha namna hiyo kwa mara ya kwanza kilifanyika Bagamoyo tarehe 9 na 10 Juni, 2023 na baadaye mkoani Mwanza kati ya tarehe 15 na 16, 2023 ambacho kiliwaleta Majaji na Maaafisa wengine kutoka Kanda ya Musoma, Bukoba, Shinyanga na Mwanza yenyewe.
Ametaja Vikao vingine vilivyofanyika ni Arusha tarehe 01 na 02 Disemba, 2023 ambacho kilijumuisha Kanda za Moshi, Manyara, Arusha na Tanga na Songea tarehe 9 had 12 Februari, 2024 kilichojumuisha Kanda za Songea, Mbeya, Mtwara, Rukwa, Iringa na Katavi.
Kikao kingine kilifanyika Kigoma tarehe 19 na 20 Aprili, 2024 ambacho kilijumuisha Mahakama Kuu ya Kazi Zanzibar, Kanda za Kigoma, Dodoma na Masjala Kuu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, akizungumza katika hafla hiyo, amesema kuwa kufanyika kwa Kikao Kazi Zanzibar ni kutanua uwigo wa kuhakikisha kwamba ujuzi walionao Tanzania Bara ni huo huo walionao Tanzania Visiwani ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.
“Maamuzi yetu ya WCF, kwa mfano, yasipokubalika yanaenda kwa Waziri mwenye dhamana ya kazi na yule anayelalamika asipokubaliana na hayo maamuzi yanahamia Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi. Kwa hiyo, unaona jinsi ambavyo mnyororo wa utendaji haki katika masuala ya kazi ulivyo,” amesema.
Kikao Kazi hicho kimefunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla. Kikao hicho kimeandaliwa kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha sheria na utoaji haki kazi Tanzania.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar (juu na chini) wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri wakati wa ufunguzi wa Kakao Kazi hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni