Ijumaa, 19 Julai 2024

WANACHAMA WA TAWJA WAKUMBUSHWA MAJUKUMU YAO

Na Daniel Sichula – Mahakama Mbeya

Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Mhe. Barke Mbaraka Sehel  amewakumbusha wanachama wa Chama hicho kuendelea kutoa michango ya uanachama ili kusaidia uendeshaji wa shughuli za Chama.

Akiongoza kikao cha wananchama wa TAWJA mikoa ya Mbeya na Songwe kilichofanyika hivi karibuni Mahakama Kuu Mbeya na kuhudhuriwa na wanachama kutoka mikoa hiyo Mhe. Sehel alisema, michango ya wanachama ndiyo nyenzo pekee ya uendeshaji wa Chama, pia alichukua fursa hiyo kuzishuru Taasisi rafiki zinazojitolea kukiwezesha Chama ikiwemo ufadhili wanaoupata kutoka Mahakama ya Tanzania. 

“Tunashukuru ufadhili tunaoupata kutoka Mahakama ya Tanzania na tunaomba muendelee na moyo huo wa kujitolea, pia kwetu wanachama tujitahidi kufanya usajili ili kushiriki makongamano mbalimbali yanayoandaliwa na Chama na Taasisi rafiki,” alisema Jaji Sehel.

Aidha, Mhe. Sehel akitoa ufafanuzi juu ya suala la kuadhimisha Miaka 25 ya TAWJA mwakani 2025, maadhimisho yakayofanyika kitaifa Jijini Arusha, alisema shughuli zote za maadhimisho hayo zitafanyika kuanzia tarehe 19 Januari, 2025 mpaka siku ya kilele tarehe 25 Januari, 2025.

Vilevile, Mhe. Sehel aliwakumbusha wanachama wa TAWJA kusajili kwa umoja wao ili waweze kujumuika kwenye fursa mbalimbali zinazojitokeza kama vile makongamano ya kimataifa ili kurahisisha chama kusaidia wanachama watakao shiriki kulingana na bajeti yake. Wakati huo huo, Mhe. Sehel aliwasihi wanachama kujitokeza kwa wingi kufanya usajili mapema ili kushiriki kongamano la kimataifa litakalo fanyika nchini South Africa jijini Durban.

Kwa upande wao wanachama wa TAWJA Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya walimshukuru Mhe. Sehel kwa mchango wake wa kukilea chama hicho na kumtunuku zawadi mbalimbali na kumuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ustawi wa Chama. Pia wananchama hao waliahidi kushiriki kwenye maadhimisho ya miaka 25 yatakayo fanyika mwakani jijini Arusha.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Mhe. Barke Mbaraka Sehel (katikati) mara baada ya mkutano wa wanachama wa chama hicho Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Mhe. Barke Mbaraka Sehel (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa mwakilishi wa wanachama hicho. 

Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Mhe. Barke Mbaraka Sehel (mbele) akiongoza mkutano wa chama hicho.


Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Mhe. Barke Mbaraka Sehel akiendesha kikao mara baada ya kuitimisha vikao vya Mahakama ya Rufani Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni