- Aimwagia sifa Mahakama uboreshaji wa miundombinu
Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini jana tarehe 11 Julai, 2024 alitembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini hapa kujifunza na kujionea mambo mbalimbali.
Mhe. Sagini alipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, kisha akapata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za kiutendaji zinazoendelea.
Naibu Waziri alitembelea baadhi ya miundombinu na maeneo, ikiwemo Ofisi za Viongozi na watumishi wa Mahakama katika jengo hilo.
Akiwa ofisini kwa Mtendaji Mkuu, Mhe Sagini alipata wasaa wa kupokea maelezo mafupi ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo la Makao Makuu lenye thamani ya billioni 129 za Kitanzania, ikiwa fedha kutoka mapato ya ndani.
"Nakushuru sana Naibu Waziri kwa kuja kututembelea, ujio wako ni faraja kwetu sisi watumishi tunaotoa huduma katika jengo hili, ni matumaini yetu shughuli zote za kiutendaji kwa watumishi wa Mahakama upande wa Makao Makuu zitaendelea kushamiri," alisema Prof. Ole Gabriel.
Alisema kuwa matokeo ya ujenzi wa jengo hilo ni ushirikiano mzuri uliopo katika ya Mihimili mitatu ya Dola na kuongeza kuwa Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu mbalimbali ya Mahakama ili kuwa na mazingira mazuri ya utoaji haki kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kupiga hatua kubwa, hususani katika miundombinu ya majengo na kuongeza kuwa amejifunza mambo mengi.
Aliahidi kupeleka salam nzuri kwa Wananchi pindi atakapopata wasaa wa kufanya hivyo katika ziara zake.
Mhe. Sagini pia alielezea kufurahishwa na mpangilio wa utendaji kazi wa Mahakama na kusema kuwa, ni mfano mzuri wa kuigwa.
"Hakika nimependezwa na uzuri wa miundombinu ya jengo hili, namna ambavyo limejengwa na kupangiliwa, ama kwa hakika hiki ni kitu kizuri sana, nimejifunza mengi kupitia ziara hii," alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni