Jumatatu, 22 Julai 2024

TUMIENI ELIMU MLIYOIPATA KAMA NYENZO YA KUISAIDIA JAMII - JAJI NKWABI

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, amewataka wanafunzi waliohitimu masomo yao kutoka Chuo cha Mafunzo Kigoma kutumia ujuzi na weledi wa elimu waliyopata ili kutoa huduma katika jamii watakayokwenda kwakuwa jamii ina matarajio makubwa juu ya wasomi wanaoendelea kuhitimu katika Vyuo mbalimbali.

Mhe. Nkwabi aliyasema hayo tarehe 19 Julai, 2024 kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 23 ya Chuo cha Mafunzo Kigoma yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho. 

Aidha, Jaji Nkwabi alisema kuwa, Mahakama Kanda ya Kigoma ipo tayari kushirikiana na Chuo hicho katika kuwajengea uwezo wanafunzi wa kozi mbalimbali ikiwemo ya Sheria kwa vitendo katika chuo hicho ambapo alisema kuwa, Maafisa Mahakama watapata muda wa kufundisha mada mbalimbali za Sheria pamoja na huduma za Mahakama ikiwa ni kutekeleza mpango mkakati wa Mahakama wa kutoa elimu kwa umma.

Alisema kuwa, Mahakama Kanda ya Kigoma imeridhia ombi la Chuo hicho la kupokea wanafunzi wa mafunzo ya sheria kwa vitendo kwa kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuendesha mashauri mahakamani kwa njia za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na jinsi Mahakama zinavyoendesha usikilizwaji wa mashauri.

Kadhalika, Mhe. Nkwabi alichukua fursa hiyo kuwakaribisha  pia mahakamani hapo kusikiliza mashauri yanapoendeshwa ili kupanua uelewa wao na kuja kuwa wasomi wazuri hapo baadae na kuwa Majaji na Mahakimu wenye weledi mkubwa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Nkwabi alikipongeza Chuo hicho na kusema, “napongeza Chuo na Uongozi wake kwa hatua za uboreshaji wa Miundombinu ya Majengo na yakufundishia wanafunzi wa kozi za afya na hata kukitangaza chuo kwa jamii inayoleta idadi hii ya wanafunzi wanaohitimu kozi hizi kwa hakika mnastahili pongezi nyingi sana.”

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Mafunzo Kigoma, Bruda Louis Kusaya, alisema kuwa, katika sherehe ya mahafali hayo jumla ya wahitimu 331 wamehitimu katika kozi sita za Sheria, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Famasia, Uuguzi na Ukunga, Afisa Tabibu na TEHAMA ambao wote wamepikwa vema katika Taaluma zao. 

“Kwa niaba ya Chuo natoa shukrani kwa Mahakama Kanda ya Kigoma kuridhia maombi yetu ya ushirikiano ya kuwajengea uwezo wanafunzi wetu katika kusoma Sheria kwa vitendo katika Mahakama zote Mkoani hapa, tunaahidi ushirikiano mkubwa wa Kitaasisi katika kukuza na kushirikiana kwa manufaa ya jamii yetu,” alisema Bruda Kusaya.

Chuo cha Mafunzo Kigoma kinamilikiwa na Shirika la Mabruda wa Upendo wa Kanisa Katoliki, kilipata usajili wa kudumu mwaka 2005 kutoka Baraza la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTEvet) na kupata ithibati kamili (Full Acreditation) Mwaka 2016. 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akitoa hotuba kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Augustine Rwizile wakati wa mahafali ya 23 ya Chuo cha Mafunzo Kigoma yaliyofanyika tarehe 19 Julai, 2024.

Sehemu ya Wahitimu wa Chuo cha Mafunzo Kigoma wakisikiliza kwa makini hotuba ya  Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi katika mahafali hayo ambaye alimuwakilisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akiwa katika Mahafali ya 23 ya Chuo cha Mafunzo Kigoma yaliyofanyika mkoani humo hivi karibuni.

Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akitoa zawadi ya cheti kwa moja ya Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi katika Wizara ya Katiba na Sheria ya Chuo cha Mafunzo Kigoma, Bi. Adilia Cleophace Kamtupe kwa uongozi bora alioufanya akiwa Waziri wa Wizara hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. John Francis Nkwabi (katikati)  akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Shirika la Mabruda wa Upendo wa Afrika na Msimamizi wa Chuo cha Mafunzo Kigoma, Chrisantus Rwehikiza (kulia) na kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Mafunzo Kigoma, Bruda Louis Kusaya.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni