Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Ujumbe kutoka Mahakama ya Juu ya Malawi umekiri kupata zaidi ya kile walichotarajia baada ya kupatiwa mada mbalimbali za namna ambavyo Mahakama ya Tanzania inavyoendesha na kuboresha shughuli za utoaji haki kwa wananchi.
Akizungumza jana tarehe 22 Agosti, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Vizano jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo yaliyojumuisha Ujumbe kutoka Mahakama ya Juu ya Malawi na Mahakama ya Tanzania ya namna ambavyo Mahakama nchini inavyofanya kazi na ilivyofanikiwa kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Malawi, Bi. Edith Chikagwa alisema mada zote zilizowasilishwa ziliandaliwa vizuri na kutoa picha ya zaidi walichotarajia.
“Mafunzo haya yatabaki kuwa miongoni mwa kumbukumbu muhimu kwa Mahakama ya Malawi, ziara yetu ilijikita kuangalia masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na namna ambavyo Mahakama ya Tanzania ivyojiendesha lakini tumepata zaidi ya kile tulichokusudia kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa, hakika tumepata zaidi ya kile kilichotuleta,” alisema Bi. Chikagwa.
Mtendaji Mkuu huyo aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kukubali ombi la kuja kujifunza na kwa namna ambavyo walivyopokelewa tangu walipowasili nchini.
Aliongeza kuwa, yote waliyojifunza watayawasilisha katika uongozi wa Mahakama yao na kuona namna ya kufanya kama ilivyofanya Mahakama ya Tanzania ili kuboresha zaidi huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
“Kupitia mafunzo haya ya kujifunza na kubadilishana uzoefu, nasi tunaahidi kwenda kuboresha huduma zetu kwa kuyatenda yote mazuri tuliyojifunza,” alieleza Bi. Chikagwa.
Akitoa hotuba ya kufunga kikao hicho cha mafunzo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Victor Kategere alisema kuhitimishwa kwa mafunzo hayo kusiwe mwisho wa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Juu ya Malawi bali uwe mwanzo wa kuendeleza ushirikiano.
Bw. Kategere alitoa rai kwa ujumbe huo kuwa Mahakama ya Juu ya Malawi kuwa, wao kama watafsiri sheria jukumu lao katika eneo la utoaji haki ni muhimu na kwamba ili kuhakikisha jukumu hili linatekelezwa ni muhimu kuajiri watumishi wa Mahakama na wasio wa Mahakama ambao kwa pamoja watatimiza jukumu hilo.
Alisisitiza pia kuhusu matumizi ya Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa shughuli za Mahakama ambapo alisema, “kutokana na kukua kwa teknolojia, Mahakama ya Tanzania ni mfano wa Taasisi ambayo inafanya shughuli zake kwa kutumia TEHAMA.”
Kaimu Mtendaji Mkuu huyo, alitaja Mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambayo Mahakama inaitumia ambayo ni pamoja na Mfumo wa Kielektroniki wa Kusimamia na Kuratibu Mashauri (e-CMS), Mfumo wa Kielektroni wa Mawakili (e-Wakili), Ofisi Mtandao (e-Office), Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS), Mfumo wa Taarifa za Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania (TanzLII) na mingine.
Ujumbe huo kutoka Mahakama ya Juu ya Malawi ambao uliwasili nchini tarehe 17 Agosti, 2024 ulipata fursa ya kupata mafunzo ya siku nne (4) ya kubadilishana uzoefu kutoka kwa wenyeji wao Mahakama ya Tanzania kuanzia tarehe 19-22 Agosti, 2024 katika Hoteli ya Vizano jijini Dodoma.
Katika siku ya mwisho ya mafunzo hayo mada kadhaa ziliwasilishwa ambazo ni Utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za Mahakama, Huduma za Maktaba na Mfumo wa Taarifa za Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania (TanzLII) Taratibu za manunuzi ndani ya Mahakama ya Tanzania, Utoaji Habari, Elimu na Mawasiliano sambamba na Itifaki ndani ya Mhimili huo.
Baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, Mahakama ya Tanzania iliwapatia washiriki wote wa mafunzo hayo kutoka Mahakama ya Juu ya Malawi Vyeti vya mafunzo kuhusu maboresho ya Mahakama ya Tanzania sambamba na ngao za pongezi kwa kutembelea Mahakama ya Tanzania na kujifunza maboresho na shughuli za Mahakama nchini.
Kadhalika Mahakama ya Juu ya Malawi walitoa zawadi kwa wenyeji wao Mahakama ya Tanzania.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Victor Kategere (kulia) akimpatia ngao ya pongezi Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Malawi, Bi. Edith Chikagwa kwa kutembelea Mahakama ya Tanzania na kujifunza maboresho na shughuli za Mahakama nchini.
Mmoja wa Wajumbe kutoka Mahakama ya Juu Malawi akipokea cheti na ngao ya pongezi kwa kutembelea Mahakama ya Tanzania na kujifunza maboresho na shughuli za Mahakama nchini.
Zoezi la utoaji vyeti kwa wageni kutoka Mahakama ya Juu ya Malawi likiendelea.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Mahakama ya Juu ya Malawi, Bi. Naomi Kwerani akifurahia cheti na ngao ya pongezi kwa kutembelea Mahakama ya Tanzania na kujifunza maboresho na shughuli za Mahakama nchini.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni