Ijumaa, 23 Agosti 2024

MTENDAJI MKUU AMJULIA HALI MAJERUHI AJALI YA BASI LA MAHAKAMA

Na Stephen Kapiga-Mahakama Mwanza. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel hivi karibuni alifika katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya kumjulia hali mtumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Bw. Jackson Kaindoa ambaye ni Afisa usafirishaji wa Busi la Mahakama  lilipata ajali ya kugongana uso kwa uso na basi la abiria linalofanya safari zake kutoka jijini Mwanza kuelekea mkoani Tabora wakati akiwapeleka watumishi kazini majira ya alfajiri ya tarehe 13 Agosti, 2023. 

Akiwa Hospitalini hapo Mtendaji Mkuu, Prof. Ole Gabriel alimweleza mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando Dkt. Fabian Masaga kuwa, ameridhishwa na taarifa ya namna uongozi wa Hospitali na Madaktari walivyoshughulikia majeruhi wa ajali hiyo na kuhakikisha wanapata matibabu ya haraka na ya uhakika ili kuwarejesha katika hali zao.

“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima na madakatari wa Hospitali ya Bugando kwa huduma nzuri na za haraka mlizoweza kuwapatia majeruhi wote wa ajali hiyo na pia matibabu mnayoendelea kumpatia mtumishi wetu hapa, hii inanipa moyo kuwa ataweza kupona kwa wakati kutokana huduma bora anyopatiwa hapa” alisema Prof. Ole Gabriel.

Aidha, ajali hiyo iliyotokea siku ya tarehe 13 Agosti, 2024 majira ya saa kumi na mbili asubuhi ilihusisha busi lilikuwa limebeba watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza lenye namba za usajili STL 1683 aina ya TATA iliyokuwa ikitokea njia ya Buhongwa kugongana uso kwa uso na basi la abiria lifanyalo safari zake kati ya Mkoa wa Mwanza na Tabora la Kampuni ya Mtoto Gema aina ya Scania lenye namba za usajili T 442 DDT. 

Chanzo ajali hiyo ilikuwa mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi la abiria la kampuni ya Mtoto Gema lilokuwa likijaribu kuyapita mabasi mengine yaliyokuwa yamelitangulia katika eneo la Mkolani jijini Mwanza na hivo kushindwa kulimudu basi hilo na kupelekea kuligonga basi lililokuwa limebeba watumishi hao waliokuwa wakielekea kazini.

Katika ajali hiyo, jumla ya majeruhi saba (7) walipatiwa matibabu na kuruhisiwa  kutoka hospitalini siku hiyo hiyo isipokuwa dereva wa basi hilo la Mahakama ambaye alipata majeraha makubwa ikiwemo kuvunjika kwa mguu wake wa kulia na kutoka kwa unyayo wake wa kukanyagia katika mguu.

Mtendaji Mkuu Prof. Ole Gabriel aliongozana na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya mwanza Bw. Tutubi Deo Mangazeni kufika hospitalini hapo na walipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando Dkt. Fabian Masaga na kumpeleka katika wodi aliyolazwa mtumishi huyo kwa ajili ya matibau zaidi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyechuchuma) akimjulia hali Bw Jackson Kaliondoa (aliyekaa kwenye kiti cha kusukumia wagonjwa) pembeni yake ni Dkt. Fabian Masaga Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya Bugando walipofika kumjulia hali majeruhi huyo.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyenyoosha mikono) akizungumza na mtumishi huyo alipokuwa wodini kumjulia hali.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akiongozana na mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya Bugando Dkt. Fabian Masaga kuingia katika wodi aliyolazwa mtumishi wa Mahakama ya Tanzania Bw Jackson Kaiondoa aliyelazwa katika hospitali ya kwa matibabu yaliyotokana na ajali ya busi.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni