· Katibu Apongezwa kwa Usimamizi Mzuri wa Rasilimali
· Sekretarieti ya Tume na Mahakama ya Tanzania wapongezwa
kwa kazi nzuri.
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameongoza kikao cha
kawaida cha Tume ambacho pia kimempongeza Katibu wake Prof. Elisante Ole Gabriel kwa
usimamizi mzuri wa rasilimali uliopelekea Tume kupata hati safi ya ukaguzi kwa
mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Aidha, kikao
hicho cha Tume pia kimeipongeza Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama
ya Tanzania kwa kazi nzuri iliyofanyika katika kipindi hicho.
Akizungumza mara baada ya
kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 31 Julai, 2024 jijini Dar
es salaam, Katibu wa Tume na Mtendaji Mkuu wa Mahakama alisema kikao hicho pia
kilijadili taarifa ya utekelezaji
wa bajeti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama (Fungu 12) na Mahakama (Fungu 40) kwa
kipindi cha Mwaka wa fedha uliomalizika wa 2023/2024.
Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Tume, Prof. Ole
Gabriel alisema katika kipindi hicho, Tume ilimshauri Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuhusu uteuzi wa Majaji 24 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Msajili Mkuu wa Mahakama, Msajili
wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu. Pia, katika kuimarisha
utendaji wa Mahakama, Tume ilimteua Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Naibu
Wasajili 30 Katibu wa Jaji Mkuu na
kuwathibitisha katika cheo Viongozi 49 baada
ya kumudu vema majukumu yao.
Alisema Tume pia iliwathibitisha kazini watumishi 207 na kupandisha vyeo watumishi 2,361 wa kada mbalimbali pamoja na
kwabadilisha Kada watumisih 124
waliopata sifa. Aidha, katika kipindi
hicho Tume iliajiri watumishi wa Mahakama 112
katika kada mbalimbali.
Kuhusu
Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama, alisema katika kikao hicho, Tume
ilipokea taarifa kuwa katika kuimarisha utendaji wa Kamati hizo, Mafunzo ya Uratibu na Usimamizi wa Kamati za
Maadili ya Maafisa Mahakama kuhusu uendeshaji wa Mashauri ya Maadili na Nidhamu
yalifanyika katika Mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Mwanza, Mara, Manyara na Arusha
yakiwa na lengo la kuzijengea uwezo Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama
kuhusu njia bora ya kushughulikia mashauri ya nidhamu yanayowasilishwa kwenye
vituo vyao.
Alisema,
waliojengewa uwezo walikuwa ni
Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa
Wilaya na Mawakili wa Serikali.
Aidha, Katibu wa Tume alisema kwa mujibu wa taarifa hiyo,
katika utekelezaji wa bajeti ya
Mwaka wa Fedha 2023/24, maeneo yaliyopewa kipaumbele ni uharakishaji utatuzi wa
mashauri ya kawaida na mkakati wa kumaliza
mashauri ya muda mrefu (Backlog),kuboresha mifumo ya teknolojia ya
habari na mawasiliano (TEHAMA) kama nyenzo muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma
na kuimarisha uwezo katika ukaguzi na usimamizi wa shughuli za Mahakama;
Aliyataja maeneo mengine kuwa ni kuimarisha maendeleo ya
rasilimali watu, ikiwa ni pamoja na mafunzo, na nidhamu ya watumishi, kuongeza
ushirikiano na wadau wa haki jinai ili kuharakisha huduma ya utoaji haki;
kuendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama
katika ngazi mbalimbali.
”Kukamilika kwa
ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali nchini, kumesogeza
kusogeza huduma za Mahakama karibu na Wananchi na kuwapunguzia wananchi gharama
ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Haki”, alisema.
Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni maboresho ya
Matumizi ya TEHAMA katika huduma
zinazotolewa na Mahakama mfano: Kukamilika na kuanza kutumika Mfumo mpya wa usimamizi wa
mashauri na kuendelea kufanya udhibiti na ufuatiliaji wa mifumo ya e-project management, e-library, e-wakili,
e-courtbroker na process server na Judicial portial na ujenzi wa kituo cha kusimamia na kuratibu mwenendo wa
mifumo na miundombinu ya TEHAMA (Judiciary Virtual Situation Room-VSR).
Kikao cha Tume kilihudhuriwa na Makamishna
watano wa Tume ambao ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.Mustapher Siyani, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ,Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi. Wengine ni Bw. Bahame Tom Nyanduga
(Wakili wa kujitegemea) na Bi.Dosca
Mutabuzi (Wakili wa kujitegemea).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni