- Awahimiza Viongozi kulinda imani waliyopewa
- Ataka haki kwenda na wajibu
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amempongeza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza nguvu Mahakama ya Rufani na kuteua Viongozi wengine ambao wanaigusa Mahakama kutokana na shughuli zao.
Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo leo tarehe 15 Agosti, 2024 kwenye hafla ya uapisho wa Viongozi mbalimbali, akiwemo Mhe. Dkt. Elieza Mbuki Feleshi baada ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Uapisho huo umefanyika katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na Mahakama, akiwepo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Hassan Zungu na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka.
Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu amewaomba Viongozi hao kulinda imani kubwa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewapa kwa niaba ya Wananchi. Jaji Mkuu aliwakumbusha kuwa imani huwa inakopeshwa kwanza kwa kuendelea kuilinda au kuipoteza.
“Hii imani ndiyo itakuwezesha kutekeleza sheria na kanuni kwa sababu utakuwa unasukumwa na ile imani katika ustawi wa Wananchi wa Tanzania,” Mhe. Prof. Juma amesema.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa changamoto kubwa katika nchi zinazoendelea siyo mapungufu ya sheria wala bajeti au Taasisi, bali watu wenyewe ambao ama wamepewa kazi ya kutekeleza au kulengwa na sheria na kuwa na tabia na tamaduni binafsi ambazo mara nyingi zinapoteza malengo mazuri yanayotarajiwa.
“Mtakapoenda kwenye sehemu zetu za kazi, pamoja na kuangalia sheria ni lazima tuangalie nafsi zetu wenyewe kama tuna tabia ambazo zinafanya sheria zisiweze kufanya kazi,” amesema.
Mhe. Prof. Juma alitumia fursa hiyo pia kueleza kuwa katika nchi zinazoendelea huwa wanasisitiza zaidi haki, lakini husahau kutimiza wajibu kwa kila mmoja.
“Kuna watu wameshajitokeza kwamba sasa hivi tunatawaliwa zaidi na haki lakini tunasahau kwamba demokrasia inajengwa zaidi kwa kuwajibika mwenyewe. Mwananchi ambaye una haki unawajibu pia kwa nchi na Taasisi yako,” amesema.
Jaji Mkuu akawaomba Viongozi hao watakapoenda kwenye maeneo yao ya kazi kuangalia haki bila kusahau wajibu walionao.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Feleshi alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi ambayo aliitumikia tangu tarehe 12 Septemba, 2021.
Kwa sasa, wadhifa huo unachukuliwa na Bw. Hamza Johari ambaye ameteuliwa na Rais Samia akitokea kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe.Dkt. Feleshi alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo alitumikia nafasi hiyo kuanzia tarehe 2 Juni, 2018.
Kama Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Feleshi alishiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika usimamizi wa Mahakama na maboresho yaliyoongozwa na Mahakama chini ya uongozi wa Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania.
Jaji Feleshi alifanya kazi kwa karibu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu wa Mahakama na wajumbe wengine waandamizi wa Mahakama katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2015/16–2019/20 kuelekea Utoaji wa Huduma za Haki unaowazingatia Wananchi. Aidha, alishiriki kufanyia kazi Mpango Mkakati wa sasa wa Mahakama wa 2020/21–2024/25.
Mhe. Dkt. Feleshi alikuwa pia Jaji wa Mahakama Kuu kuanzia Agosti, 2014 hadi Septemba, 2021 ambapo alifanya kazi katika kituo cha Dar es Salaam kuanzia Agosti, 2014 hadi Februari, 2017; Masjala ya Iringa kuanzia Februari, 2017 hadi Juni, 2018 na Masjala Kuu kuanzia Juni, 2018 hadi Septemba, 2021.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 15 Agosti, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni