Ijumaa, 16 Agosti 2024

UJENZI MAHAKAMA ZA MWANZO TATU RUKWA WAIVA

Na MAYANGA SOMEKE–Mahakama, Sumbawanga

Ujenzi wa Mahakama za Mwanzo tatu katika Mkoa wa Rukwa utaanza hivi karibuni baada ya Mahakama ya Tanzania kukabidhi maeneo ya miradi hiyo kwa Mkandarasi, Bw. Nassir Mohamed kutoka kapuni ya Skywards Co. LTD.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga, Bw. Machumu Essaba alikabidhi maeneo hayo kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania, tukio ambalo lilishuhudiwa na Wawakilishi kutoka Makao Makuu ya Mahakama na Viongozi wengine.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Essaba alimhimiza Mkandarasi huyo na Mshauri Mwelekezi, kutekeleza makubaliano ya mkataba wa ujenzi wa Mahakama hizo Nambogo, Kasanga na Namanyere ili ziweze kukamilika kwa wakati.

Mahakama ya Mwanzo Nambogo itajengwa katika Wilaya ya Sumbawanga, Mahakama ya Mwanzo Kasanga itajengwa katika Wilaya ya Kalambo na Mahakama ya Mwanzo Namanyere itajengwa katikaWilaya ya Nkasi.

Mtendaji huyo alieleza kuwa Wakandarasi Wazawwamekuwa wakipokelewa vizuri baada ya kuaminiwa na kupelekwa kwenye miradi kwa ajili ya utekelezaji wa mikataba, lakini wamekuwa wakishindwa kwenda na mpango kazi waliowasilisha wao wenyewe, badala yake huleta visingizio endelevu na kuchelewesha ujenzi.

“Hali hii hatutaivumilia wala hatutaikubali kwa muda wote tutakaosimamia miradi, pasiwepo na neno changamoto kwenye majadiliano yetu yote mpaka kukamilisha kwa miradi,”alisema.

Alieleza kuwa hawatasita kumjulisha Mshauri msimamizi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa maandishi kufuta mara moja kandarasi hiyo kwenye mkoa wa Rukwa kama wataona dalili za kusuasua kwa mradi na viashiria vyovyote vya kwenda nje na mpango kazi.

Naye Mshauri wa Majengo(Consultancy) kutoka Kampuni ya NORPLAN(T) LTD, Bw.Elton Maroalisema miradi yote mitatu itakwenda kwa pamoja na itadumu ndani ya miezi sita kuanzia tarehe 12 Agosti, 2024.

Bw.Maro alisema kwamba, Mkandarasi huyo amepewa siku 14 ya kufanya maandalizi ya vifaa vya ujenzi pamoja rasilimali watu na atatakiwa kukamisha mradi mwezi Februari, 2025 na kukabidhi Mahakama hizo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za haki.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Sumbawang,a Bw. Machumu Essaba  akiwa Pamoja na wageni katika ofisi yake.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Sumbawang,a Bw. Machumu Essaba na Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Norplan(T) LTD, Bw. Elton Maro wakimkabidhi nyaraka za kiwanja cha NambogoWilaya ya Sumbawanga Mkandarasi, Bw. Nassir Mohamed kutoka Kampuni ya Skywards Co. LTD.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga, Bw. Machumu Essaba na Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Norplan(T) LTD, Bw. Elton Maro akimkabidhi nyaraka za kiwanja cha KasangaWilaya ya Kalambo Mkandarasi, Bw. Nassir Mohamed kutoka Kampuni ya Skywards Co. LTD.

Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba na Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Norplan(T) LTD, Bw. Elton Maro akimkabidhi nyaraka za kiwanja cha NamanyereWilaya ya Nkasi Mkandarasi, Bw. Nassir Mohamed kutoka Kampuni ya Skywards Co. LTD.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni