Ijumaa, 16 Agosti 2024

MAHAKIMU ARUSHA WANOLEWA NAMNA YA UENDESHAJI MASHAURI YA UKATILI WA KINGONO

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama - Arusha

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba amefungua mafunzo ya kuzuia athari kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono na kijinsia ili kuwajengea uwezo Mahakimu wa mkoani humo juu ya namna bora ya kushughulikia mashauri yanayohusu wahanga wa ukatili wa kingono na kijinsia kuanzia ngazi ya familia.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo jana tarehe 15 Agosti, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, Mhe. Mwaseba alisema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni pamoja kutoa uelewa wa namna matukio hayo yanavyoripotiwa katika Vituo vya Polisi na yanavyoendeshwa Mahakamani.

“Moja ya malengo ya mafunzo haya ni kuwawezesha Mahakimu wanaosikiliza mashauri haya kupata uelewa wa kutosha juu ya namna nzuri ya kusaidia kutotonesha vidonda kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia,” alisema Mhe. Mwaseba.

Aliongeza kwamba, mafunzo hayo yanawaandaa pia washiriki kuboresha uelewa wao juu ya mashahidi ambao ni wahanga wa ukatili wa kingono na kijinsia ikiwa ni pamoja na sheria zinazowalinda watu hao na kujifunza mbinu za kuendesha mashauri ya jinsi hiyo. 

Aidha, mafunzo hayo pia yanaangazia uendeshaji wa mashauri ya kimaadili, matumizi ya teknolojia katika kusaidia ushahidi na usimamizi bora wa mashauri ili kuzuia athari hasi kujirudia kwa wahanga wa unyanyasaji wa kingono.

Lengo lingine la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa, kila mshiriki anapata maarifa na ujuzi wa kuendesha mashauri ya unyanyasaji wa kijinsia kwa ufanisi na kuzingatia haki ikiwa ni pamoja na kulinda utu na haki za wote wanaohusika katika shauri husika.

Watoa mada katika mafunzo hayo ni jumla ya Mahakimu nane ambao walipatiwa mafunzo ya namna hii awamu ya kwanza kwa lengo la kuwawezesha Mahakimu wenzao. Mafunzo hayo yanafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia jana tarehe 15 hadi 16 Agosti, 2024.

Mafunzo ya namna hii yalitolewa awali kwa Mahakimu Wakufunzi wa mkoani Arusha kuanzia tarehe 03 hadi 05 Juni, 2024 kwa lengo la kuwapa maarifa ili nao wawafundishe Mahakimu wengine. Mafunzo hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania, Serikali ya Tanzania na Shirika la Kimataifa la Utawala wa Sheria la Ireland.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba akifungua mafunzo ya kuzuia athari hasi kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha jana tarehe 15 Agosti, 2024. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Ayoub Mwenda na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Erasto Philly.
 
Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mkufunzi, Mhe. Neema Mchomvu akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa mafunzo ya kuzuia athari hasi kwa wahanga wa ukatili wa kingono na kijinsia yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha kuanzia tarehe 15 hadi 16 Agosti, 2024. 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu Arusha mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya 
kuzuia athari kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono na kijinsia. Walioketi wa pili kulia ni  Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Ayoub Mwenda, wa pili kushoto ni  Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Dkt. Dafina Ndumbaro, wa kwanza kulia ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Erasto Philly. Waliosimama ni Sekretarieti ya mafunzo hayo, katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Mhe. Theresia Sedoyeka, kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Josephine Mshanga na kulia ni Hakimu Mkazi na Mratibu wa Mafunzo, Mhe. Julieth Mbise.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu Arusha pamoja na washiriki wa mafunzo ya kuzuia athari hasi kwa wahanga wa ukatili wa kingono na kijinsia yanayofanyika kuanzia tarehe 15-16 Agosti, 2024 (IJC) Arusha. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni