Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jumla ya Wanafunzi 109 wa kidato cha tatu na Walimu watano kutoka Shule ya Sekondari Mikamba iliyopo wilayani Kasulu walitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma hivi karibuni na kukiri kuridhishwa na kufurahishwa na elimu waliyopata sambamba na namna Mahakama hiyo inavyotoa huduma.
Akitoa elimu kwa wanafunzi hao walioonesha kuhamasika kujifunza kuhusu huduma za Mahakama na shughuli zake za kila siku, Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina aliwafundisha Muundo wa kila Mahakama ili wafahamu uwezo wa Mahakama husika, Mamlaka zake na jinsi zinavyofanya kazi.
Mhe. Kagina aliwaeleza kuwa, Mahakama Kuu Kigoma ndio Mahakama inayopokea mashauri yote ya rufaa kutoka Mahakama za chini pamoja na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba (DLHT) na Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa Mkoa huo.
Aliongeza kuwa, katika jengo hilo, ipo Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufaa ambayo inashughulikia rufaa zote kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Bw. Ramadhani Kufakunoga aliwaeleza wanafunzi hao kuhusu jengo la kisasa linalotumika na Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma na kuwajuza kwamba, jengo hilo lina ghorofa mbili zikitanguliwa na ghorofa ya chini ambayo ndio yenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma na kwamba ndio ilipo sehemu ya awali ya kupokea wateja wote wanaokuja hapo kupata huduma za Mahakama.
“Jengo hili linayo mifumo mbalimbali ya kidijitali inayowezesha kuendesha mashauri kwa njia ya picha jongefu (Virtual Court) iliyopunguza gharama za wateja kusafiri umbali mrefu kuja kupata huduma za kusikilizwa mashauri yao, badala yake hubaki Mahakama za Wilaya wanakotoka na kuunganishwa kwa mfumo huo na kusikiliza kesi zao zilizopo hapa Mahakama Kuu,” alisema Bw. Kufakunoga.
Aidha, wanafunzi hao pamoja na Walimu walipitishwa Mahakama ya Watoto (Juvenile Court) ambayo ni maalum kwa ajili ya watoto wanaokwenda kinyume na Sheria ya Mtoto.
Wanafunzi hao walielezwa kuwa, Mahakama zinapokuta watoto wamekosea huadhibiwa kwa mujibu wa Sheria hiyo na kupelekwa katika Shule ya Maadilisho.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Taaluma kutoka Shule ya Sekondari Mikamba, Bw. Robson Aron Gwahila, aliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma kwa ukaribisho na kuwawezesha kupata elimu ya sheria na huduma za Mahakama.
Bw. Gwahila alisema wataendelea kutembelea Mahakama hiyo ili kujifunza maana wanao wanafunzi ambao bado wanahitaji kupata elimu hiyo wanapofika kila hatua ya masomo yao.
Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa kidato cha tatu na Walimu kutoka Shule ya Sekondari Mikamba. Kushoto kwa Mhe. Kagina ni Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Mikamba, Bw. Robson Gwahila na kulia kwake ni Mwalimu Augustino Lyaheja pamoja na Walimu wengine walioambatana na wanafunzi wa Shule hiyo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni