Na CHARLES NGUSA-Mahakama, Geita.
Jumla ya watumishi 15 kutoka Mahakama ya Rufani Tanzania wameshiriki katika mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita kwenye ziara iliyofanyika hivi karibuni.
Watumishi hao waliongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Agatha Chugulu ambapo malengo ya ziara hiyo ilikuwa ni kujifunza namna bora ya uendeshaji wa mashauri na shughuli zingine za kiofisi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA).
Awali akizungumza na watumishi hao baada ya kuwasili katika Mahakama hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina alisema “Geita kwa sasa hatutumii karatasi katika shughuli zetu za uendeshaji wa mashauri na shughuli zingine za kiofisi kama vile shughuli za kiutawala ambazo zote zinafanyika kwa kupitia mfumo wa kusajili mashauri(CMS) na ofisi mtandao ,hivyo kwa kiasi kikubwa tumeweza kuepuka matumizi ya karatasi kabisa na kuokoa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kilikuwa kinatumika kununua shajara na badala yake fedha hizi kuelekezwa katika motisha za watumishi wetu ili kuwaongezea morali ya kufanya kazi.”
Watumishi hao, waliweza kupitishwa katika ofisi mbali mbali na kuoneshwa namna shughuli zinavyoendeshwa katika Mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na ofisi inayotumika kwa ajili ya “Visual court” pekee ambapo Mhe. Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe.Fredrick Lukuna alisema “chumba hiki ni kwa ajili ya kuendeshea mashauri kwa njia ya mtandao yaani “Visual Court “ hivyo hakuna shughuli nyingine inayofanyika. Katika chumba hiki huwa tuna Tv kubwa ambayo kwa mfano labda nyie huko mnaweza kuwa na shahidi yuko huku kwetu hivyo mkiwasiliana nasi tunamwita anaingia katika chumba hiki na anaendelea kutoa ushahidi wake bila wasiwasi.”
Aidha, watumishi hao baada ya kumaliza kupitia katika kila ofisi waliweza kuingia ukumbi wa Mahakama ambapo walijifunza mambo mbalimbali ikiwemo mchakato mzima wa ufunguaji wa mashauri mpaka kufikia hatua ya mwisho.
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Lukuna aliwaeleza kuwa mchakato unaanza kwa wakili au ofisi ya mashitaka na pengine kupitia kiosiki cha Mahakama kwa wale ambao hawana barua pepe (email) au hawana wakili hivyo hulazimika kuja kwenye kiosiki cha Mahakama kusaidiwa kupandisha nyaraka zao kwenye mfumo na kutumwa kwenda kwa Msajili kwa ajili ya kufanyiwa usajili.
Mhe. Lukuna aliongeza kwamba baada ya shauri kutoka kwa msajili kama ni la madai, huelekezwa kwenda uhasibu kwa ajili ya kutoa namba ya malipo yaani ‘control’namba kwa ajili ya kulipia na baadae kwenda kwa Mhe. Jaji Mfawidhi kwa ajili ya kupangiwa Jaji na upangaji wa mashauri hufanywa na mfumo wenyewe.
Mhe .Msajili alieleza kuwa katika Mahakama hiyo hawapokei nyaraka ngumu bali wanapokea pokea nakala laini pekee ambazo zinakuja kupitia mfumo wetu na kufanyiwa kazi isipokuwa tu kama mteja hana wakili na wala barua pepe, hivyo huwasilisha nyaraka zake kwenye kiosiki ili ziweze kupandishwa kwenye mfumo na kuendelea na utaratibu wa kawaida.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao waliokuja kujifunza, Mkuu wa msafara huo, Mhe.Chugulu amepongeza juhudi zinazoendelea katika Kanda hiyo na kuwashukuru kwa namna ambavyo wameweza kuwa Mahakama ya mfano katika matumizi ya TEHAMA na kwamba wamejifunza mengi na wataenda kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza ili kuboresha huduma katika maeneo yao ya kazi.
Baada ya hapo watumishi hao wakiongozwa na wenyeji wao waliweza kutembelea eneo la mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Geita ambalo ni kwa ajili ya Mahakama Jumuishi na kwamba kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kuboresha huduma katika Kanda hiyo, kwani huduma
zote zitakuwa zinapatikana katika jengo hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni