Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amewataka wadau wa haki kazi kujenga na kuimarisha mfumo jumuishi unaosomana ili kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa michakato mbalimbali katika utatuzi wa migogoro ya kazi.
Mhe. Siyani ametoa wito huo leo tarehe 22 Agosti, 2024 katika Ukumbi wa PSSF Millenium Tower jijini Dar es Salaam alipokuwa anafungua mkutano wa kamati ya utatu wa wadau wa haki kazi ambao umeandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.
“Ni muhimu sana kuwa na mfumo jumuishi wa haki kazi unaosomana baina ya Mahakama na wadau, utakaosaidia kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa michakato mbalimbali katika utatuzi wa migogoro ya kazi kati ya wadau watatu muhimu; Serikali, Waajiri, na Wafanyakazi.
“Mfumo huu utaimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya wadau wa utatu, kuhakikisha kuwa haki za kazi zinalindwa na migogoro inatatuliwa kwa wakati stahiki,” amesema katika mkutano ambao umehudhuriwa na Majaji Wafawidhi kadhaa wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na wadau wengine kutoka Taasisi zinazoshughulikia masuala ya kazi.
Jaji Kiongozi amebainisha kuwa eneo la haki kazi, haliwezi kukwepa au kubaki nyuma katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki kwa kuzingatia nyakati zilizopo sasa zilizoathiriwa na mapinduzi ya nne ya viwanda, ambapo mifumo ya utendaji kazi inategemea zaidi matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Aliwaeleza washiriki kuwa mkutano huo utawapa fursa ya kuangalia ni namna gani wanaweza kujenga na kuimarisha mfumo jumuishi wa haki kazi unaosomana baina ya Mahakama na wadau.
Mhe. Siyani amesema kuwa mfumo jumuishi wa kieletroniki na matumizi ya TEHAMA utawarahisishia wafanyakazi na waajiri kupata habari kuhusu haki zao na utaratibu wa kutatua migogoro baina yao.
Amesema kwamba kupitia mifumo ya aina hiyo, sekta nyingi duniani zimefanikiwa, ikiwemo wafanyakazi au waajiri kuweza kuwasilisha malalamiko au kutafuta msaada bila vizuizi vinavyohusishwa na mifumo ya zamani, kama vile mapungufu ya kiuchumi, kijiografia au ucheleweshaji unaosababishwa na urasimu.
“Mimi naona mifumo hii kama mwarobaini wa changamoto nyingi zinazotukabili. Ninaamini, mfumo jumuishi wa kielektroniki na matumizi ya TEHAMA wa haki kazi, utarahisisha pia mchakato wa kufungua malalamiko na kusimamia kesi…
“Ufanisi huu utapunguza muda wa kutatua migogoro na kudumisha maelewano maeneo ya kazi, ikiwemo kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanapata haki zao mapema iwezekanavyo,” amesema.
Aidha, Jaji Kiongozi ameeleza kuwa mfumo jumuishi utawawezesha wadau wote kupata habari kuhusu kesi zinazoendelea na uwazi huo utasaidia kujenga imani kati ya wadau kwa kuhakikisha kuwa michakato iko wazi na hivyo kuongeza uwajibikaji.
Mhe. Siyani ameeleza pia kuwa matumizi ya mfumo jumuishi wa kielektroniki na matumizi ya TEHAMA utaruhusu ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu zinazohusiana na migogoro ya kazi.
“Takwimu hizi ni muhimu kwani zinaweza kutoa taswira ya mwenendo wa mahusiano sehemu za kazi na kusaidia watunga sera kutambua matatizo ya kimfumo yanayohitaji kushughulikiwa...
“…Kwa kupitia hayo, Serikali inaweza kuboresha kanuni na mifumo. Mfumo jumuishi wa kielektroniki utakuza mawasiliano bora kati ya Serikali, Waajiri, na Mashirika ya Wafanyakazi. Aidha utasaidia majadiliano na mazungumzo, kufanyika kwa urahisi na kufikia makubaliano juu ya maswala yanayoathiri wafanyakazi na waajiri,” amesema.
Kadhalika, Jaji Kiongozi ameeleza kuwa katika usikilizaji wa mashauri ya kazi, mfumo jumuishi wa haki kazi utatuwezesha upatikanaji wa kumbukumbu za mashauri kielekroniki kwa ngazi zote za vyombo vya utoaji haki kazi kama Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, jambo litakalopunguza muda wa uendeshaji na gharama kwa wadau.
Awali, akizungumza wakati akimkaribisha Jaji Kiongozi kufungua mkutano huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina, alisema kuwa mkutano huo ni wa nane wa kamati ya utatu wa wadau ambao unafanyika kwa mujibu wa kanuni 7 (2) ya Tangazo la Serikali namba 209 la 2010.
Alisema kuwa kwa mujibu wa tangazo hilo, kamati inapaswa angalau kuwa na kikao kimoja kwa mwaka na hujumuisha wawakilishi kutoka katika makundi makuu matatu, yaani wawakilishi wa wafanyakazi, wawakilishi wa waajiri na Serikali.
Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa mkutano huo una lengo la kuwaleta wadau wote muhimu katika kuibua, kujadili na kuamua kwa pamoja mambo yanayohusu haki kazi.
“Kwa mikutano saba iliyopita, kamati ya utatu imeshuhudia mafanikio makubwa yatokanayo na mikutano hii. Mikutano iliyopita imekuwa nguzo imara ya mafanikio yetu.
“Kwa kupitia mikutano iliyotangulia, wadau walikubaliana mambo yaliyoonekana kukwamisha kazi miongoni mwetu kutokana na kutekeleza kwa pamoja kila Taasisi majukumu yake, tumeweza kusikiliza na kuamua kwa wkati mashauri ya kazi,” Mhe. Dkt. Mlyambina alisema.
Alibainisha kuwa mzingo wa mashauri unazidi kupungua kila siku na kazi ya kumaliza mashauri inaongezeka na tena kwa muda mfupi. Jaji Mfawidhi alisema pia kuwa wamefanikiwa kuchapisha majuzuu ya maamuzi ya Mahakama ya Rufani kwenye mashauri ya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani.
Naye Mkurugezi wa Chama cha Waajiri Tanzania, Bi. Suzan Doran Ndomba, akizungumza baada ya ufunguzi was mkutano huo, ameeleza kuwa uwepo wa mfumo jumuishi katika haki kazi ni jambo ambalo wamekuwa wakilililia kwa muda mrefu.
“Tunafahamu kwamba Mahakama imekwenda mbali zaidi kwenye masuala ya teknolojia na kwa sasa hivi hii itakwenda kuboresha utoaji wa haki kwa wakati. Pale ambapo mifumo itakuwa inasomana itawezesha wadau kuwasilisha mashauri kwa wakati na haraka zaidi, nafikiri hili ni jambo jema na sisi tunalifurahia sana,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Mhe. Usekelege Nashon Mpulla alisema kuwa suala la mfumo siyo tu ni msisitizo wa Mahakama, bali pia wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kurahisisha utendaji kazi na utoaji haki.
“Mifumo ya Taasisi zote isomane ili kumwezesha mwananchi kuhudumiwa kwa urahizi zaidi. Sisi kama CMA, tunafahamu Mahakama tayari imeshaanzisha huo mfumo…
“…kwa maelekezo ya Serikali, Tume inatekeleza mradi kuhusu Mfumo wa Utatuzi wa Migogoro na Usajili. Kupitia mradi huu, waajiri na waajiliwa wataweza kusajili mashauri yao kwa njia ya kielekitroniki popote pale walipo na sisi tutaishughulikia kwa haraka,” alisema.
Mkutano huo una kauli mbiu isemayo “Wajibu wa Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo wa Haki Kazi kwa Ustawi wa Taifa”. Katika mkutano huo, mada mbalimbali zitawasilishwa kuwakumbusha wadau wa haki kazi namna ya kutekeleza wajibu wa kila mmoja.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mkutano wa katmati ya utatu wa wadau wa haki kazi leo tarehe 22 Agosti, 2024 jijini Dar es Salaam.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina akitoa neno wakati wa kufungua mkutano wa utatu wa wadau wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya kazi.
Sehemu ya Wasaidizi wa Majaji wa sheria kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi wakiwa wanachukua hadidu rejea za mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni