Na AHMED MBILINYI – Mahakama, Bukoba
Makabidhiano ya eneo kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Izigo katika Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera yalifanyika hivi karibuni na kushuhudiwa na Wawakilishi kutoka Makao Makuu ya Mahakama na Viongozi wengine.
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza tarehe 17 August, 2024. Viongozi walioshuhudia makabidhiano hayo ni Mhandisi Peter Mrosso, Mkadiriji Majenzi (QS) Deogratius Lukansola, Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko na Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Muleba, Mhe. Daniel Nyamkerya.
Wengine ni Afisa Tawala Mwandamizi Mahakama Kuu Bukoba, Bw. Rojas Rwanyumba, Afisa Utumishi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Muleba, Bi. Edventina Semba, Msanifu Majenzi Mshauri (Consultant), Bw. Shempemba Elibariki kutoka Kampuni ya Norman and Dawbarn, Mkandarasi, Bw. Laurent Ambros pamoja na timu yake Kutoka kampuni ya Clalon Technologies.
Mwenyekiti wa kikao hicho cha makabidhiano, Msanifu Majenzi, Bw. Elibariki alielezea kuwa mradi huo ni wa muda wa miezi sita na utaanza rasmi tarehe 17 August, 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 16 February, 2025.
Bw. Elibariki alimesisitiza mambo mbalimbali kwa Mkandarasi wa Mradi, ikiwemo kuzingatia muda kwani mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Benki ya Dunia. Alisema pia kuwa uzalishaji taka uzingati kanuni zake katika kuziharibu.
Msanifu Majenzi pia alimsisitiza Mkandarasi kuzingatia mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wake pamoja na vibarua atakaowatumia, kujisajili Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), kutembelea Ofisi ya Manispaa kuonana na Mhandisi wa Manispaa na kuwaona Idara ya Zimamoto kabla ya kuanza shughuli za ujenzi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba aliahidi kuwapa ushirikiano Wakandarasi na kufanya mawasiliano na Taasisi zote zinazohusika kutoa vibali ndani ya Mkoa wa Kagera.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni