Na Innocent Kansha- Mahakama
Mkuu wa Idara ya Itifaki Kitaifa Mhe.
Balozi Yusuph Mndolwa amesema kuwa itifaki ni suala mtambuka la utaratibu
unaokubalika wa kufanya mambo kwa heshima na tabia njema jambo ambalo linapaswa
kuanzia ngazi ya familia, jamii ya watu wastarabu, taasisi, mihimili na hata kitaifa
katika misingi inayoheshimisha utu na hadhi za viongozi.
Akizungumza katika kikao kazi cha
kujadili masuala ya itifaki kilichowahusisha Majaji wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania kilichofanyika jijini Dar es salaam leo tarehe 02 Septemba, 2024
Balozi Mndolwa amesema kuwa kuna baadhi ya taratibu zimekuwa zinafuatwa na
zingine kufuatwa katika misingi isiyo ya ukamilifu wa kiitifaki.
Mhe. Balozi Mndolwa amewakumbusha
Majaji hao juu ya mambo kadhaa ya kiitifaki kwa kuzingatia utaratibu
unaokubalika bila kumkwaza aliyealikwa na aliyealika mambo hayo ni pamoja na
mavazi ya staha, ukaaji na mpangilio wa nani aanze na nani afuate, kuzingatia
vyeo, tabia za mezani pamoja na mawasiliano mbalimbali, mambo hayo ndiyo msingi
wa tabia njema za kiitifaki.
“Mavazi ya staha na rangi kwa watumishi
wa umma ni vitu vinavyotambulisha watu wa fani fulani kama Majaji na watu wa
kanda mbalimbali za watumishi wa umma, mfano kwa upande wa wanaume tuepuke sana
kuvaa tai nyekundu kwani rangi nyekundu inamaanisha mamlaka,” amesema Mhe.
Balozi.
Mhe. Balozi Mndolwa akagusia itifaki ya
ukaaji kwa Waheshimiwa Majaji na Watendaji wa Mahakama wakati wamealikwa kwenye
hafla na dhifa mbalimbali za mhimili na zingine za kitaifa na serikali. Amesema
kwamba eneo hilo lina
changamoto sana na linahitaji kufanyiwa
mkakati mahususi wa kuondoa mtanziko huo. Njia moja wapo ni sekretarieti
inayoandaa dhifa kushirikiana na viongozi wa mihimili mingine kushauriana namna
ya ukaaji wa kufuata hadhi za wageni walioalikwa.
“Changamoto nyingine ya kiitifaki ni
namna ya ukaaji kwenye picha, kuna picha nyingine ukiiangalia tu inakueleza
kuwa hapa mpangilio hakufuata itifaki. Picha ni historia hivyo ni lazima
itifaki kuzingatiwa ili kulinda historia,” ameongeza Mhe. Mndolwa.
Mhe. Balozi Mndolwa
akizungumzia matumizi ya simu za mikononi, ametoa rai kuwa wakati wote mgeni
anapaswa kuzingatia mahali alipo na watu aliokuwa nao. Mtu anapokuwa kwenye
hafla au dhifa ya aina yoyote ile itifaki inashauri kuweka simu kwenye sauti
ndogo ama mtetemo ili kuondoa usumbufu.
Mhe, Balozi Mndolwa akizungumzia eneo
la utoaji wa mialiko ya dhifa mbalimbali za serikali na kitaifa amesema
kumekuwa na changamoto ya watu kutothibitisha ushiriki wao kwa maandishi ili
kuwawezesha waandaaji kuratibu shughuli husika kwa ufasha kuanzia mapokezi,
ukaaji kwa kuzingatia uthibitisho wa wageni husika. Itifaki inashauri kuwa
mwalikwa anapaswa kutoa uthibitisho wa kushiriki katika muda uliokusudiwa ili
kurahisisha shughuli nzima ya itifaki.
Kuhusu matumizi ya pasi za kusafiria
zenye hadhi ya kibalozi, Balozi Mndolwa amesema Majaji na watendaji wa Mahakama
na wenza wao wanaruhusiwa kisheria kutumia pasi hizo za kusafiria. Lakini wakati
mwingine wahusika wamekuwa wamekuwa wakitumia hadhi hiyo kinyume na utaratibu
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya
Rufani ya Tanzania Mhe. Augustine Gherabast Mwarija akifungua kikao kazi hicho
amewataka Majaji hao kusikiliza Balozi huyo kwa umakini ili waweze kutoa
michango mizuri hasa ya kuuliza maswali kwenye maeneo mbalimbali yanayotokana
na changamoto za itifaki.
Mkuu wa Itifaki na Adabu Kitaifa Mhe. Balozi Yusuph Mndolwa (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili masuala ya itifaki na ustarabu kilichowahusisha Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kilichofanyika Mahakama ya Rufani jijini Dar es salaam leo tarehe 02 Septemba, 2024
Mkuu wa Itifaki na Adabu Kitaifa Mhe. Balozi Yusuph Mndolwa (aliyenyoosha mikono) akifafanua jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili masuala ya itifaki na ustarabu kilichowahusisha Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kilichofanyika Mahakama ya Rufani jijini Dar es salaam leo tarehe 02 Septemba, 2024
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ambaye pia ni mlezi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Augustine Gherabast Mwarija (katikati) akifungua kikao kazi hicho kilichowahusisha Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania walioshiriki kikao kazi hicho wakisikiliza kwa umakini hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni