Jumatatu, 2 Septemba 2024

MAHAKAMA, WADAU NJOMBE WAKUTANA KUBADILISHANA UZOEFU

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe imefanya kikao pamoja na wadau wake katika Mkoa huo wakiwemo Baraza la Ardhi Mkoa, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na wanafunzi wa Vyuo vya Sheria lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu kwa ustawi wa utoaji haki kwa wakati mkoani humo.

Kikao hicho kilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na kuongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho.

Akifungua kikao hicho, Mhe. Chamshama aliwakaribisha wadau waliofika kwenye kikao hicho, ambapo alisema, “tumewaalika kwenye kikao hiki ili tuweze kubadilishana uzoefu kwa kupata elimu mbalimbali hasa kutoka kwenye Mabaraza kujua shughuli hasa zinazofanywa nanyi mkiwa huko nanyi muweze kujua shughuli tunazozifanya sisi kama Mahakama.” 

Katika kikao hicho Mwenyekiti alipokea taarifa mbalimbali za utendaji kazi kutoka kwa wadau wa Mahakama huku akitoa elimu kwa hoja zilizokuwa zinaibuka kwenye kikao hicho pamoja na kujibu maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na wanafunzi kutoka Vyuo mbalimbali vya Sheria huku akisisitiza matumizi ya TEHAMA ambayo yamerahisisha ufanyaji kazi za kimahakama na kupunguza mzunguko uliokuwa unajitokeza. 

Mhe. Chamshama aliwasisitiza Mawakili wa mkoani Njombe kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kwamba kama wana mashauri katika Mkoa wowote siyo lazima wasafiri bali wafike mahakamani hapo kupata huduma hiyo. 

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Amos Singo alitoa elimu kuwa, wao kama CMA wanahusika kutatua migogoro ya kazi, na kwamba wana Taasisi mbili ambazo ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi pamoja na Idara ya Kazi.

Bw. Singo alisema kuwa, Idara ya Kazi ina jukumu la kwenda kukagua kwenye maeneo ya kazi kujiridhisha kwamba taratibu za kisheria zinafuatwa kama zilivyowekwa, jukumu jingine ni kukagua kama mfanyakazi anakuwa na mkataba wa ajira lakini pia kuangalia mahitaji yote ya kisheria ya mfanyakazi anayopaswa kuwa nayo/kuyapata kama vile likizo, masuala ya muda wa kazi yanazingatiwa.

Naye, Mwakilishi kutoka Baraza la Ardhi Bwana Godfrey Msunga, alisema kuwa migogoro mingi inayoenda Baraza inatokana na kurithi maeneo ambapo Mahakama inashindwa kutatua kwa warithi wa maeneo kwa kuwa hawana nyaraka za uthibitisho hasa kwenye suala la mirathi linapokuja mahakamani.

Pamoja na hilo, Bw. Msunga alitoa nasaha kwa wananchi kuhakikisha unakuwa na hati ya ardhi sambamba na kulipia kodi ya ardhi huku akieleza kwamba kuwa na vielelezo ni muhimu kwakuwa inarahisisha utoaji haki kwa wakati na kuepusha changamoto.  

Wakili wa Kujitegemea Mwandamizi, Bw. Frank Ngafumika pamoja Wakili aliyewakilisha ofisi ya TAKUKURU walitoa neno la kuwahasa Mawakili wenzao kuwa na nidhamu na uadilifu katika kazi zao kwa kufuata taratibu na kuwa na umoja ili waweze kufanya kazi kwa pamoja na kutochukiana kisa kesi wanazozisimamia mahakamani.

Pamoja na hayo, Mawakili hao waliipongeza Mahakama kwa maboresho mengi yaliyofanyika huku wakilinganisha zamani na sasa ambapo walieleza kuwa katika kipindi hiki Mahakama inasikiliza mashauri kwa wakati na kufuata sheria. 

Naye Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Njombe Mjini, Mhe. Barnaba Mwangi aliwasihi Mawakili  kuzingatia  utaratibu wa kupokelewa  mahakamani na kuthibitisha kuwa ni kweli ameajiriwa na  mteja kwa ajili ya kusimamia shauri lake ili kuepukana na migogoro na wateja wao mahakamani.

Kadhalika Mhe. Mwangi alizungumzia kuhusu taratibu za mirathi, majukumu ya msimamizi wa mirathi kwenye mchakato wa kufunga mirathi ambapo alisema mirathi ni njia mojawapo ya watu kumiliki mali na kuthibitisha mahakamani kwa kupewa na mtu anayesimamia mirathi aliyeteuliwa mahakamani au kutekeleza wosia uliotolewa mahakamani.

Alizungumzia pia kuhusu changamoto za Mawakili wanapokuja kusajili mashauri ya mirathi kwa Mahakama za Mwanzo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao  kati ya Mahakama na Wadau kilichofanyika katika Mahakama hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita. Kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Njombe Mjini, Mhe. Barnaba Mwangi na kulia ni  Mdau kutoka  Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Amos Singo.

Mdau kutoka  Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Amos Singo akitoa elimu kwa wadau wengine (hawapo katika picha ) kuhusu kazi zinazofanywa na CMA.

Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Lupembe, Mhe. Godfrey Msemwa (aliyesimama) akiuliza swali kwa wadau wakati wa Kikao kati ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe pamoja na Wadau wake. 

Hakimu Mkazi, Mhe. Isack Mlowe akisikiliza swali lililokuwa linaulizwa kutoka kwa wadau (hawapo katika picha).

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Makete, Mhe. Irvan Msacky (aliyesimama) akichangia hoja pamoja naye ni baadhi ya wadau kwenye picha kwa pamoja.

Picha ya juu na chini na Mahakimu , Mawakili wa Serikali na wa Kujitengemea pamoja na wanafunzi kutoka Vyuo vya Sheria kwa pamoja wakisikiliza mada zilizokuwa zikitolewa kwenye kikao cha pamoja kati ya Mahakama mkoani Njombe na Wadau wake. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni