Jumatatu, 2 Septemba 2024

JAJI MFAWIDHI DODOMA ASISITIZA UBUNIFU KAZINI

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo amesisitiza watumishi kuwa wabunifu kazini ili kuongeza ufanisi katika kazi zao. 

Mhe. Dkt Juliana alitoa rai hiyo hivi karibu katika kikao na watumishi wakati akikabidhi zawadi kwa mtumishi, Bw.Stansalaus Makendi ambaye ni Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi, baada ya kuibuka kinara wa kutumia mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS).

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mkutano uliopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.

“Ningependa kutoa zawadi hizi kwa kila mtumishi, hii iwe motisha na kwa wengine mfanye kazi kwa bidii na kuwa wabunifu katika kazi zenu, kwani kutapelekea na kuongeza ufanisi mkubwa kwenye kazi na hata nje ya kazi pamoja na kujiepusha na vishawishi vya rushwa, tutimize majukumu yetu,” alisema.

Naye Bw. Makendi aliwashukuru watumishi kwa zawadi hizo walizompatia pamoja na ushirikiano wao.

Kikao hicho kilichoundwa na wajumbe ambao ni watumishi wa Kanda hiyo ya Dodoma ambacho hufanyika kila siku ya Ijumaa asubuhi kiliazimia kutekeleza na kusimamia kwa ukaribu masuala mbalimbali.

Baadhi ya masuala hayo ni kutumia vyema mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama inavyosisitizwa na Viongozi wa juu, kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama, hasa Mahakama za Mwanzo, kusikiliza mashauri kwa wakati ili kutovuka mwaka na mlundikano .

Sambamba na hayo, Jaji Mfawidhi aliwakumbusha watumishi kuendelea kutekeleza maelekezo mbalimbali ya Viongozi, likiwemo maelekezo ya utoaji nakala ya hukumu siku ya kusomwa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo (juu na chini) akionyesha zawadi kabla ya kuikabidhi kwa mhusika katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa IJC Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo (juu na chini) akikabidhi zawadi kwa Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi, Bw.Stansalaus Makendi wakati wa kumpongeza katika kikao hicho.



Baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma (juu na chini) wakiwa katika picha ya pamoja  wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo (wa pili kutoka kushoto).



 Picha yzawadi ambazo amekabidhiwa Bw.Stansalaus Makendi(hayupo kwenye picha).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni