Na PAUL PASCAL -Mahakama Moshi
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi hivi karibuni ilifanya mafunzo kwa watumishi na wadau wa Mahakama 55 kuhusu Mfumo wa Kieletroniki wa Kuratibu, Kusikiliza na Kusimamia Mashauri “Advanced electronic Case Management System” (e-CMS) ili kuongeza uelewa.
Mafunzo hayo yaliwaleta pamoja Mahakimu, Wasaidizi wa Kumbukumbu, Mawakili wa Serikali,Mawakili wa Kujitegemea na Maendesha Mashtaka kutoka TAKUKURU, KINAPA, UHAMIAJI pamoja na maofisa wa Magereza.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Moshi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella amesema matumizi ya mfumo huo ulioboreshwa utasaidia utunzaji wa taarifa kieletroniki na kuharakisha uendeshaji wa mashauri.
“Ikumbukwe kuwa mafunzo haya sio ya mara ya kwanza katika Kanda yetu. Tunarudia kuyafanya kwani tumebaini changamoto kwa watumiaji wengi wa mfumo. Niwatake kwa umoja wetu katika mnyororo wa utoaji haki tubainishe changamoto zote ili tuelekezane na mmoja wetu asibakie nyuma,” alisema.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mafunzo Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Safina Simfukwe aliwaalika washiriki kuainisha changamoto anazokutana nazo katika utendaji wake ili wazitumie kuelimishana kadiri itakavyowezekana.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje alitoa rai kwa washiriki wote kuwa makini wakati wote wa mafunzo ili kupata matokeo chanya.
“Niwaombe wote tuungane pamoja na kusikilizana kwa makini ili tunapotoka hapa kila mmoja awe na uwezo wa kuutumia mfumo pasipokuwa na kikwazo, naamini hilo linawezekana kwa utayari wetu,”alisema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt, Lillian Mongella akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watumishi na wadau wa Mahakama (hawapo pichani).
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mratibu wa Mafunzo, Kanda ya Moshi, Mhe. Safina Simfukwe(aliyee simama) akiongea wakati wa mafunzo hayo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje (aliyesimama) akiwakaribisha wadau katika mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa wazi Mahakama Kuu Moshi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni