Jumanne, 3 Septemba 2024

JAJI MKUU ATAKA USHIRIKIANO KIMATAIFA KUPAMBANA NA UHALIFU WA KUPANGWA

Na FAUSTINE KAPAMA - Mahakama, Dar es Salaam 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 3 Septemba, 2024 amefungua warsha ya wadau wa haki jinai ili kujadiliana nafasi ya Sheria katika kupambana na makosa ya uhalifu wa kupangwa wa kuvuka mipaka, yakiwemo ya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, dawa za kulevya na uhalifu mitandaoni.

Mhe. Prof. Juma amefungua warsha hiyo ya siku mbili inayofanyika katika Hoteli ya White Sands Resort jijini Dar es Salaam ambayo imewaleta pamoja wadau zaidi ya 80 wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu Wakazi Wakuu, Waendesha Mashtaka, Wataalamu na Wawakilishi mbalimbali wa Vyombo vya Usimamizi wa Sheria na Taasisi za Kifedha kutoka Tanzania, Msumbiji na Kenya.

Vyombo hivyo vya usimamizi wa Sheria na Taasisi za Umma ni Mamlaka za Kupambana na Dawa za Kulevya, Uhalifu Mitandaoni, Uchunguzi wa Jinai wa Kimaabara, Benki Kuu ya Tanzania, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jumuiya ya Mabenki Tanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzu wa washa hiyo, Jaji Mkuu ametoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa Kimataifa na wa pamoja kati ya Mataifa ili kukabiliana na uhalifu wa kupangwa wa kimataifa barani Afrika, hususan; Kenya, Tanzania na Msumbiji.

"Tunahitaji ushirikiano, hatuwezi kusimama peke yetu dhidi ya uhalifu wa kupangwa wa kimataifa," amesema.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kupambana na uhalifu uliopangwa wa kimataifa, kama vile biashara ya binadamu, biashara ya madawa ya kulevya, uvuvi haramu, uharamia na wizi wa kutumia silaha, pamoja na biashara ya silaha.

Amesema kuwa madhara ya uhalifu wa kupangwa kimataifa yanaonekana katika nchi kama Kenya, Tanzania na Msumbiji, kwani kila moja inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na uhalifu huo kutokana na maeneo ya kijiografia, hali ya uchumi wa kijamii na mazingira ya kisiasa.

"Hatuwezi kushinda vita dhidi ya uhalifu uliopangwa wa kimataifa, ikiwa tutajificha nyuma ya uhuru wetu wa kitaifa," Jaji Mkuu alimewaambia washiriki katika warsha hiyo.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Jaji Mkuu kufungua washa hiyo, Jaji wa Mahakama ya RufaniTanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Dkt. Paul Faustine Kihwelo alisema uhalifu wa kupangwa wa kimataifa unaingilia aina mbalimbali za uhalifu unaovuka mipaka ya kijiografia.

Kwa ajili hiyo, alisema mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa kimataifa siyo yale ambayo yanaweza kushinda kwa Taasisi au taifa moja pekee bali yanahitaji juhudi za pamoja za wadau wote. 

Warsha hiyo imeandaliwa na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya sheria ya Maendeleo (IDLO) na itadumu kwa siku mbili hadi tarehe 04 Septemba,2024.

Katika warsha hiyo wadau hao watajadiliana jinsi ya kuimarisha ushirikiano na ushirikishwaji miongoni mwao  katika ngazi za kitaifa na kikanda,  na pia kutafakari juu ya kubadilishana taarifa, uzoefu, changamoto, na mbinu bora za kukabiliana na Uhalifu wa Kimataifa uliopangwa miongoni mwa nchi hizo tatu.

Aidha, warsha hiyo inalenga kutafakari na kupitia mapendekezo yanayotokana na Kongamano la wadau wa Mahakama la kujadili makosa ya uhalifu wa kifedha lililofanyika Januari 2024 jijini Dodoma ambalo liliwapa wadau dhana na maarifa muhimu ili kukabiliana kwa ufanisi dhidi ya Uhalifu huo wa Kimataifa uliyopangwa.













 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni