Jumatano, 4 Septemba 2024

JAJI KIONGOZI MAHAKAMA KUU TANZANIA AWAAPISHA NAIBU WASAJILI WATANO WAPYA

  • Awataka kutimiza majukumu yao bila woga
  • Awaonya kuwa watapimwa kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amewataka Naibu Wasajili kutekeleza majukumu yao katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa wananchi bila woga, chuki, huba wala upendeleo.

Mhe. Siyani ametoa wito huo leo tarehe 4 Septemba, 2024 baada ya kuwaapisha Naibu Wasajili wapya watano, Mhe. Rose Ernest Kangwa, Mhe. Sophia Salum Massati, Mhe. Aloyce Evarist Katemana, Mhe. Hudi Majid Hudi na Mhe. Daudi Peter Kinywafu, katika halfa iliyofanyika ofisini kwake Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu jijini Dar es Salaam.

“Nyinyi kama askari wa haki msiwe waoga. Uoga kwa watumishi wa Mahakama, hususan wa ngazi zenu ni vitu ambavyo havitaiwezesha Mahakama kutimiza jukumu lake la kikatiba. Ndiyo maana mmekula viapo vya kutokuwa na uoga na kutoyumbishwa mnaposimamia haki...

“Nataka wote mkumbuke kuwa, kama mtapaswa kuwa na hofu au woga, basi iwe kwa Mwenyezi Mungu. Lakini timizeni majukumu yenu bila hofu kama iliyo kwa askari. Askari anapoenda vitani anajua kinachoweza kutokea, lakini anakwenda.”

Jaji Kiongozi amesisitiza jambo hili mara kwa mara katika hotuba yake kwa Viongozi hao la kutokuwa na hofu wanapotimiza majukumu yao na kuwahimiza kuchapa kazi bila huba au chuki, huku wakijua kuwa watapimwa kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.

“Nendeni mkaviishi viapo vyenu na kuzitendea haki nyenzo mnazopewa kwa nafasi zenu. Daima kumbukeni mambo matatu yanayojenga salamu ya Mahakama na kila wakati mnatakiwa kukumbuka mambo hayo matatu; uadilifu, weledi na uwajibikaji,” amesema.

Mhe. Siyani amewakumbusha kuwa Naibu Wasajili na Mahakimu Wafawidhi ndiyo askari wa Mahakama pale linapokuja suala la utoaji haki kwa wakati. 

Amebainisha kuwa katika suala la utoaji haki, Mahakama haitumii bunduki wala vifaru, wala silaha nyingine yoyote, bali inategemea watu na watendaji mahiri wanaozingatia misingi ya haki.

Hivyo, Jaji Kiongozi akawahakikishia kuwa kama watakuwa waadilifu, hakuna atakayeadhibiwa kwa kutimiza wajibu wake, hivyo akawataka waende wakachape kazi bila woga wala hofu.

“Woga hautawasaidia chochote na mwoga yoyote tutamjua. Huyu mwenzetu ni askari mwoga, tumempa mamlaka atimize wajibu kwa niaba yetu, asimamie haki na sheria zipo, lakini hataki kutekeleza. Hili ni jambo linalofikirisha sana kwa Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi,” amesema.

Amewapitisha katika hotuba ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa mwaka 1964 alipohutubia halaiki ya watu waliohudhuria tamasha la gwaride rasmi la kuhitimisha mafunzo ya askari jeshi la ulinzi wa wananchi.

Katika hotuba yake, Mwalimu Nyerere alisema, “Niliapa kuwa nitafanya kazi yangu kwa uaminifu na kutimiza wajibu wangu kwa kazi hizo kwa bidii na kwa moyo mkunjufu…

“…na kwamba nitawatendea watu wote kwa mujibu wa sheria na mila za Jamhuri yetu bila woga, upendeleo, huba, au chuki. Kiapo hiki siyo cha bure, ni ahadi mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba nitajitahidi kutimiza wajibu wangu.”

Mwalimu Nyerere aliwaambia askali hao kuwa siyo watumishi wengi wanaopata nafasi, heshima na uzito wa kuapishwa kama wao. Akasisitiza kwamba kwa kiapo chao, askali wameapishwa mbele yake, wananchi wenzao na mbele ya Mwenyezi Mungu.

Aliwaeleza kuwa kiapo walichoapa siyo cha bure, ni kiapo ambacho kila mmoja atafanya kila awezalo kutimiza wajibu wake katika kulitumikia Taifa. Akawataka kamwe wasikengeuke, wakasahau kiapo chao na kwamba Tanzania inatarajia mambo makubwa matatu kutoka kwao, uaminifu, utii na uhodari.

Kisha, Jaji Kiongozi akawageukia Viongozi hao wapya na kuwaambia kuwa maneno hayo ya Mwaasisi wa Taifa yanaishi na kuakisi uhalisia katika zama zetu, japo yalitolewa zaidi ya miaka 60 iliyopita, lakini yanaakisi majukumu yaliyopo mbele yao.

Mhe. Siyani amewapongeza Viongozi hao kwa kuaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo, imani ambayo imejengwa na misingi ya uadilifu na weledi katika kusimamia, kupanga na kutoa haki, uteuzi ambao umezingatia kazi kubwa ambayo tayari wameifanya.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (juu na picha mbili chini) katika mwonekano tofauti alipokuwa anaongea na Naibu Wasajili watano wapya baada ya kuwaapisha kwenye hafla iliyofanyika leo tarehe 4 Septemba, 2024 jijini Dar es Salaam.


Mhe. Rose Ernest Kangwa akiapa.

Mhe. Sophia Salum Massati akila kiapo.

Mhe. Aloyce Evarist Katemana akila kiapo.

Mhe. Hudi Majid Hudi akila kiapo.

Mhe. Daudi Peter Kinywafu akila kiapo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akisaini moja ya kiapo baada ya uapisho.

Naibu Wasajili wapya. Kutoka kushoto ni Mhe. Rose Ernest Kangwa, Mhe. Sophia Salum Massati, Mhe. Aloyce Evarist Katemana, Mhe. Hudi Majid Hudi na Mhe. Daudi Peter Kinywafu.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria uapisho huo. Picha juu kutoka kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert. Picha chini ni sehemu ya Viongozi wengine, akiwemo Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sudi Fimbo (wa kwanza kulia) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Bi. Mary Shirima (wa pili kutoka kulia).

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja. Wengine katika picha ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi wa pili kutoka kushoto), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (wa pili kutoka kulia) na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert (wa kwanza kushoto) na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili wapya.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati)  ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali na Naibu Wasajili wapya.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Mahakama. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni