Na Innocent Kansha - Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha Naibu Wasajili na
Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi kutambua kuwa wao ni Viongozi wa Mahakama watakaowakilisha Uongozi wa Mahakama na watumishi wa ngazi mbalimbali katika majukumu
yao mapya watakayoyatekeleza maeneo mbalimbali waliyopangiwa hapa nchini.
Akizungumza
katika hafla fupi mara baada ya kuwakabidhi nyenzo za kufanyia kazi Mahakimu
Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi watano leo tarehe 04 Septemba, 2024
jijini Dar es salaam, Mhe. Prof. Juma amewambia Viongozi hao kuwa wao kazi yao
ni nyepesi iliyotajwa katika Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayosisitiza utoaji wa haki.
“Hatuna
kazi kubwa sana zaidi ya utoaji wa haki katika ngazi mbalimbali za kimahakama
na kwa bahati nzuri kuna maelekezo mengi ya namna hiyo, haki inatolewa kwa
namna gani. Mathalani kutoa haki kwa kuzingatia sheria ninaimani wote tunafahamu…
"...vilevile
kufuata kanuni za kutenda haki bila kujali hali ya mtu na bila upendeleo
kulingana na viapo vyetu, kutochelewesha haki, kujaribu kutoa fidia pale panapo
stahili na pia kutofungwa na masharti ya kiufundi na kuzingatia maadili,”
amesisitiza Jaji Mkuu.
Aidha,
Jaji Mkuu akawahimiza Viongozi hao kuwa, wakiweza kusimama katika misingi hiyo
kila jambo watakaloshughulika nalo litakwenda vizuri. Hivyo akawatakia mema na
fanaka katika kazi zao za kila siku.
Kwa upande mwingine, Mhe. Prof. Juma akawakumbusha Viongozi hao kwenda kusimamia Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania na Programu ya Maboresho ya huduma za kimahakama yanayoendelea.
Akawasisitiza Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao waliokabidhiwa nyenzo za kutendea kazi na Naibu
Wasajili walioapishwa kuwa wana kazi kubwa ya kuwa mawakala wa maboresho
kwa kuyasemea na kusimamia.
“Unajua
wananchi wanapozungumzia maboresho wanajua ni majengo tu, kumbe sisi mtaji wetu
mkubwa ni yale mambo yanayotokana na majengo, yanayotokana na mabadiliko ya
sheria, ndiyo yana faida kubwa zaidi katika maboresho kuliko yale mambo
yanayoonekana kuwa mawakala wa maboresho ni pamoja na kwenda kutenda haki,”
ameongeza Jaji Mkuu,.
Vile
vile, Jaji Mkuu amewahimiza Viongozi hao kutathimini mwelekeo
wa shughuli za Mahakama hasa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwa mabalozi wazuri katika matumizi ya mfumo mpya wa
usimamizi wa mashauri (e-Case Management System) ambao umeshaanza kufanya kazi
kwa mafanikio makubwa na programu ya kudijiti nyaraka na kumbukumbu ili kuachana
na matumizi ya karatasi, huo ndiyo mtihani mkubwa ambao Mahakama inaendelea nao.
"Tayari kuna mifano ya mafanikio kwa baadhi ya Mahakama mfano, Mahakama ya
Wilaya Kigamboni wamepiga hatua kubwa sana katika kuhama kutoka kwenye matumizi
ya kutumia karatasi (Paperless Court) katika shughuli za huduma za utoaji haki na
pia Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita vile vile hawatumii karatasi. Tukiweza
kutoka kwenye matumizi ya karatasi nadhani thamani ya haki tunayotoa itakuwa
kubwa zaidi, tutakuwa wawazi zaidi, tutakuwa na ufanisi zaidi na tutakuwa na ubora
zaidi,” ameongeza Jaji Mkuu.
Katika
hatua nyingine Jaji Mkuu amewataka viongozi hao kupenda kujisomea na
kujiendeleza hata kwa kujifunza kutoa kwa viongozi wenzao kujua wanafanya nini
katika maeneo yao kila siku wanapotimiza majukumu yao. Wanakabiliana vipi na changamoto
zinazojitokeza za kimahakama hususani kwenye vyombo vya habari na namna ya
kuzitatua.
“Kazi
yetu ni kazi ya umma kwa hiyo tukubali kukosolewa, tunaweza kukosolewa kwa haki
na vilevile tunaweza kukosolewa kwa kuonewa na siku zote huwa hatupigi kelele. Kwa
sababu mtu anayekukosoa anaweza kuwa anakukosoa kwa kutokuelewa kwa hiyo ni
jukumu lako kumelimisha na kuna wengine wanakukosoa kwa makusudi tu wakiwa wanafahamu ukweli uko wapi ila anakukosoa tu, huyo unamsamehe lakini lengo letu
ni kuhakikisha tunawafikia wananchi wa kawaida,” amesema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiteta na Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi (hawapo pichani) walioteuliwa na kuapishwa na kukabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi leo tarehe 04 Septemba, 2024 ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Hahakimu Makazi Mafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mhe. Ally Abdallah Mkama akikabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto)
Hahakimu Makazi Mafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mhe. Mwanaheri Kassim Rashid akikabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto)
Picha na Innocent Kansha- Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni