Jumatatu, 16 Septemba 2024

JAJI MKUU ATOA WITO WA KUDUMISHA AMANI ILI KUMUENZI MTUME MUHAMMAD S.A.W

Na Innocent Kansha na Tawan Salum- Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 15 Septemba, 2024 aliungana na waumini wa Dini ya Kiislam mkoani Dar es salaam kuadhimisha swala ya kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W) iliyobeba kauli mbiu isemayo mmomonyoko wa Maadili ni chanzo cha uvunjifu wa amani.

Akizungumza katika sherehe ya mazalia ya Mtume Muhammad iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma alisema ujumbe wa hafla hiyo uliobeba ujumbe wa Mtume Muhammad (S.A.W) na amani ikimaanisha kwamba ni hafla ya kutafakari maisha na mafundisho mbalimbali ya Mtume Muhammad kuhusu amani.

“Mtume Muhammad ameendelea kutuhamasisha kuwa watu wema kufanya mema na kumuabudu Mungu. Turudi tuangalie matendo ya Mtume Muhammad (S.A.W) ambayo yalimpambanua katika mazingira ya amani, matukio ya zamani ambayo yalikuwa yanasisitiza amani na mbinu alizokuwa anatumia zilikuwa za kisayansi na zenye ufanisi mkubwa zinazoweza kutumika katika karne hii ya 21 ambazo zitadumisha amani,” alisema Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Prof Juma alisema kuwa sheria zinapata nguvu kama jamii ina maadili na maadili yanapatikana katika mafundisho ya dini na hadithi za Mtume katika Kitabu Kitakatifu. Mwenyezi Mungu alituumba tukiwa na utofauti lakini ametuunganisha katika amani ambayo inatuwezesha kuishi na kushirikiana katika nchi moja ambayo ni Tanzania.

“Mtume Muhammad alikuwa na sifa zilizokuwa zinajenga amani kwa wakati huo na tukizifuata kwa sasa zitatusaidia kujenga amani katika nchi yetu. Sifa mojawapo ni ya subira, sifa hii ni ya muhimu sana unapochokozwa unahitaji subira, sifa nyingine ni usitaimilivu, uvumilivu na kupenda maridhiano ndiyo misingi wa amani,” aliongeza Jaji Mkuu.

Pia Mtume Muhammad alikuwa na hadithi nyingi zilizomtambulisha kuwa na tahadhali kabla ya kutokea kitendo chochote cha uvunjifu wa amani. Kwenye masuala ya amani tahadhari ni muhimu sana siku zote usijitayarishe kupambana na maadui zako badala yake tumia muda mwingi kumwelekea mwenyezi Mungu kuomba kwa ajili ya amani.

“Nyakati nyingine hakutakuwa na ujumbe wa amani katika mazingira yaliyokuwa na dhuluma, uonevu na ukandamizaji kushiriki katika makubaliano ambayo upande mmoja hauwezi kuyatimiza mfano; unakopa fedha mkopo unakuwa chehchefu unatafuta mbinu za kutolipa, vitendo hivyo vyote vinakuwa ni uvunjifu wa amani,” alisisitiza Jaji Mkuu

Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma akitoa mfano mwingine wa kudumisha amani aliongelea mkataba wa Madina ujulikanao kama Katiba ya Madina. Mkataba huo ulimpambanua Mtume kuwa kiongozi aliyetayari kuwaongoza watu wa dini, kabila na rangi mbalimbali waweze kuishi pamoja kama ilivyo Tanzania, “tunayo Katiba ya nchi na sheria za nchi, katiba ya nchi inatusaidia sisi tuweze kuishi kwa amani kwa umoja na ushirikiano kwa sababu tunawatu wa jamii mbalimbali,” aliongeza Mhe. Prof. Juma.

Naye, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhaji Walid Omari Kawambwa alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuitikia wito wa kuwa Mgeni Rasmi na kushiriki sherehe za kumbukizi ya mazalia ya Mtume Muhammad S.A.W.

“Nipongeze Jaji Mkuu kwa kutupenda, kutuheshimisha, kutujali lakini umetupatia kipaumbele cha hali ya juu, niwakumbushe wapenda amani wote kuwa jamii ya Tanzania ina amani na tutaendelea kubaki kuwa nchi ya amani,” aliongeza Shekhe Kawambwa.

Shekhe Kawambwa alisema kuwa, katika jamii yoyote ya kistaarabu kuishi kwa maadili ni jambo lisiloepukika na hivyo basi husaidia kuiathiri jamii moja kwenda jamii nyingine kuweza kuishi kimaadili na hatimaye nchi nzima kuwa yenye maadili na kupelekea kujiepusha nchi kukumbwa na mmomonyoko wa maadili ambao unachangia uvunjifu wa amani. 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwahutubia waumini wa Dini ya Kiislamu mkoani Dar es salaam kuadhimisha swala ya kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W) iliyobeba kauli mbiu isemayo mmomonyoko wa Maadili ni chanzo cha uvunjifu wa amani jana tarehe 15 Septemba, 2024 katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es salaam.

Sehemu ya waumini wa Dini ya Kiislamu mkoani Dar es salaam waliokutana katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es salaam kuadhimisha swala ya kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W).
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye koti la bluu) akifuatilia mawadha mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na wanazuoni wa Dini ya Kiislumu kataka sherehe za kumbukizi ya mazalia ya Mtume Muhammad (S.A.W)

Sehemu ya waumini wa Dini ya Kiislamu mkoani Dar es salaam waliokutana katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es salaam kuadhimisha swala ya kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W).

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye koti la bluu) akifuatilia mawadha mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na wanazuoni wa Dini ya Kiislumu kataka sherehe za kumbukizi ya mazalia ya Mtume Muhammad (S.A.W)

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye koti la bluu) akiongozwa na mwenyeji wake Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhaji Walid Omari Kawambwa akimpokea wakati wa hafla hiyo.


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye koti la bluu) akifurahia jambo na sehemu ya Mashekhe walioshiriki kwenye sherehe za kumbukizi ya mazalia ya Mtume Muhammad (S.A.W)

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni