Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigali
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 10 Septemba, 2024 jioni alitembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda na kushiriki chakula cha jioni kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili yake na Balozi, Mhe. Maj. Gen. Ramson Godwin Mwaisaka.
Akiwa katika ofisi za ubalozi huo, Mhe. Prof. Juma alipata taarifa mbalimbali namna watumishi wanavyofanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na jinsi ubalozi unavyoiwakilisha vyema Tanzania katika nchi hiyo.
Kadhalika, alipata maelezo jinsi ubalozi huo unavyoshirikiana na nchi hiyo katika kuendeleza mahusiano mema kati ya Tanzania na Rwanda ambayo yemeendelea kuwa mazuri na kuimarisha ushirikiano na diplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Baada ya kupata maelezo hayo, Jaji Mkuu aliongozana na mwenyeji wake kwenye eneo ambalo lilikuwa limeandaliwa kwa ajili ya chakula.
Akitoa neno la ukaribisho, Balozi Mwaisaka alimshukuru Jaji Mkuu pamoja na ujumbe wake kwa kuwatembelea na kukubali kushiriki kwenye chakula cha jioni ambacho alikuwa amekiandaa licha ya kuwa na ratiba ngumu ya ushiriki kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Jumuiya ya Madola unaondelea kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Kigali.
“Nakushukuru sana Jaji Mkuu kwa kuja kutuona na kushiriki pamoja nasi kwenye chakula hiki pamoja na ratiba yako ngumu. Ninawakaribisha sana hapa ubalozini, hapa ni nyumbani kwenu,” alisema.
Naye Jaji Mkuu alirejesha shukurani kwa watumishi wote wa Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda kwa ukarimu na chakula kizuri walichokuwa wamekiandaa, ikiwemo kaunga ambayo ni maarufu Tanzania kama ugali.
Alitumia fursa hiyo kumweleza Balozi na watumishi wote maboresho makubwa ambayo Mahakama ya Tanzania imefikia, ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Mhe. Prof. Juma alieleza pia kuwa ujenzi wa miundombinu, ikiwemo majengo ya Mahakama unaendelea kwa kasi ambapo kufikia mwaka 2025 nchi nzima itakuwa na huduma za Mahakama Kuu kwenye kila Mkoa.
Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu aliongozana na Majaji wawili wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine wa Mahakama Kuu.
Viongozi wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Katibu wa Jaji Mkuu, Katibu wa Jaji Kiongozi na Katibu wa Msajili Mkuu.
Walikuwepo pia Viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) wa ngazi mbalimbali, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania ambao wanashiriki kwenye Mkutano huo wa Kimataifa.
Sehemu ya Viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi, Mhe. Maj. Gen. Ramson Godwin Mwaisaka. Kushoto ni Makamu wa Rais, Mhe. Shaibu Mzandah na kulia ni Katibu Mwenezi, Mhe. Nemes Mombury.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni